Maandalizi ya kombe la Chan yachelewa Kenya

Timu ya Kenya Harambee Stars
Image caption Timu ya Kenya Harambee Stars

Haikuwa rahisi kwa Kenya kushinda haki za kuandaa kombe la matiafa ya Afrika 2018 Chan ambayo sasa yanawaponyoka.

Shirikisho la soka nchini humo FKF likiongozwa na aliyekuwa katibu wake Sam Nyamweya lilitumia shilingi milioni 50 mwaka 2013 kupigania zabuni ya kuandaa michezo hiyo mbali na kusimamia safari za mara kwa mara za kuelekea makao makuu ya Caf nchini Misri ili kujadiliana na maafisa wakuu wa soka barani Afrika.

Hatahivyo ombi hilo la kuandaa michuano ya 2013 lililenga kombe la mataifa ya Afrika 2017 lakini afisa mmoja wa Caf nchini Misri badala yake aliipatia Kenya haki za kuandaa dimba la Chan lisilo na umaarufu mkubwa.

kulingana gazeti la Daily Nation nchini Kenya ,Zambia pia ilikuwa imewasilisha ombi lake la michuano hiyo ya Afcon pamoja na Kenya na kupoteza kabla ya kinyang'anyiro hicho kupelekwa nchini Libya na baadaye kuandaliwa na Gabon mwaka mmoja baadaye kutokana na mgogoro wa kisiasa nchini Libya.

Wakati huo Caf ilisema kuwa Kenya ilishinda haki ya kuandaa Chan na sio Afcon ili kuweza kuisaidia Kenya kupima uwezo wake wa kuandaa michuano hiyo.

Hatua hiyo ya Caf inatokana na uzoefu wa hapo awali wa Kenya ambapo taifa hilo lilifanikiwa kupewa haki ya kuanda dimba hilo kabla ya kujiondoa dakika za mwisho kama ilivyokuwa 1986 na 1996.

Gazeti hilo linasema kuwa sasa imebainika wazi kwamba Kenya ilikuwa ikitaka kuandaa michuano ya Afcon na wala sio Chan ukiangazia hali ya taifa hilo kuweka miundo mbinu ya kuandaa dimba hilo.

Swala jingine ni kwamba barua ya kwanza ya Kenya ya kuandaa michuano ya Chan haikutoka kwa rais ama hata maafisa wakuu wa serikali kama ilivyo ada na mataifa yaliofanikiwa.