Wakamatwa India kwa kuishangilia timu ya kriketi ya Pakistan

Pakistan ilishinda fainali kwa kuitandika India kwa mikimbio 180. Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pakistan ilishinda fainali kwa kuitandika India kwa mikimbio 180.

Watu 15 wamekamatwa katika jimbo la Madhya Pradesh nchini India kwa madai kuwa waliishangilia Pakistan wakati wa fainali ya kombe la kriketi kati ya India na Pakisan

Polisi waliiambia BBC kuwa wanaume hao wa kiislamu walishtakiwa kwa kosa la kuhujumu serikali.

Walikamatwa baada ya majirani wao wa kihindu kulalamika kuwa walishangilia na kutamka maneno ya kuiunga mkono Pakistan wakati wa mechi.

Pakistan ilishinda fainali kwa kuitandika India kwa mikimbio 180. Hujuma kwa serikali ni moja ya makosa mabaya zaidi nchini India.

Watu wanaoshtakiwa kwa makosa hayo husalimisha stakabadhi zao kwa polisi, hawapewi ajira ya serikali , na ni lazima wafike mahakamani wanapohitajika na kutumia pesa kwa kesi zao.

Hii si mara ya kwanza waislamu wa India wamejikuta taabani kwa kuishangilia timu ya kriketi ya Pakistan.

Mwaka 2014 wanafunzi 66 wa kiislamu kutoka eneo la Kashmir linalosimamiwa na India, walifukuzwa kutoka chuo kikuu katika jimbo la Uttar Pradesh na kushtakiwa kwa kuvuruga umoja wa jamii.

Mada zinazohusiana