Familia ya Otto Warmbier yakataa mwili wake kuchunguzwa

Marehemu Otto Warmbier wakati alipokamatwa nchini Korea Kaskazini
Image caption Marehemu Otto Warmbier wakati alipokamatwa nchini Korea Kaskazini

Familia ya mwanafunzi wa Marekani aliyefariki muda mfupi baada ya kuachiliwa huru nchini Korea Kaskazini imekataa uchunguzi wa mwili wake kulingana na afisa anayechunguza vifo.

Otto Warmbier alifariki siku ya Jumatatu karibu na nyumbani kwaokatika jimbo la Ohio baada ya kuzuiliwa nchini Korea Kaskazini kwa zaidi ya miezi 15.

Mchunguzi mkuu wa vifo katika kaunti ya Hamilton alisema kuwa mwili wa Otto ulifanyiwa uchunguzi wa viungo vya mwili.

Korea Kaskazini inadai kwamba kukosa kwake fahamu kulisababishwa na kutiliwa sumu katika chakula na dawa ya usingizi lakini familia ya Warmbier na madaktari wamekana.

Bwana Warmbier alihukumiwa miaka 15 jela na kazi ngumu mnamo mwezi Machi 2016 baada ya kushtakiwa kwa kujaribu kuiba bango la propanganda katika hoteli moja.

Afisi ya mchunguzi wa maiti katika eneo la Cincinnati jimbo la Ohio ilisema katika taarifa: ''Hatujathibtisha sababu ya kifo cha Warmbier wakati huu kwa kuwa kuna rekodi za kimatibabu na uchunguzi mbali na watu kufanyiwa mahojiano.Huruma yetu ni kwa familia na marafiki wa Warmbier wakati huu wa msiba''.

Madaktari katika hospitali ya Cincinnati ambapo bwana Warmbier alitibiwa baada ya kurudi nchini Marekani mnamo tarehe 13 mwezi Juni, walisema kuwa aliugua ugonjwa wa kukosa fahamu baada ya kuumizwa ubongo.

Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika siku ya Alhamisi katika shule moja huko Wyoming,Ohio, ambapo Bwana Warmbier alisomea kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha Virginia.

Rais Donald Trump siku ya Jumatatu alisema kwamba bwana Warmbier alifanyiwa vitu vibaya chini ya mikono ya utawala mbaya wa Korea Kaskazini.

Mada zinazohusiana