Bunge la Uingereza kufunguliwa

Bunge la Uingereza kufunguliwa huku Malkia Elizabeth akihutubia sera za seriali ya Theresa May
Image caption Bunge la Uingereza kufunguliwa huku Malkia Elizabeth akihutubia sera za seriali ya Theresa May

Bunge la Uingereza linafunguliwa leo, katika sherehe ambayo Malkia Elizabeth, atasoma sera ambazo serikali ya chama cha Conservative cha Waziri Mkuu Theresa May kinanuia kutekelezwa

Sherehe za leo zinaonekana hazitakuwa kama za kawaida kwa misingi ya maandalizi na pia katika sera.

Badala ya kusafiri kwa gari maalum linalovutwa na farasi, na kulakiwa na gwaride la jeshi, Malkia Elizabeth leo atawasili katika majengo ya bunge kwa gari dogo.

Kinyume na utamaduni, hapatakuwepo na mavazi maalum kwa mara ya kwanza tangu 1978

Hali hii imesababishwa na uchaguzi ambao umemuacha waziri mkuu kutokuwa na idadi ya kutosha bungeni ili kuidhinisha miswada, na sasa Bi May anajaribu kuunda muungano na vyama vingine vidogo vidogo, mpango ambao umesababisha hotuba hiyo ya Malkia kucheleweshwa.

Image caption Theresa May

Matokeo hayo ya uchaguzi pia yanamaanisha Bi May atalazimika kupuuza baadhi ya sera zake ambazo hazikuwa maarufu.

Bunge la sasa litatawaliwa na mjadala kuhusu Uingereza kujiondoa kutoka kwa muungano wa Ulaya mbali na muda wa bunge hilo kuongezwa.

Serikali ya Bi May inatarajiwa kuwa na wakati mgumu bungeni, kwa kuwa hakuna serikali ambayo imewahi kushughulikia suala hili na Uingereza kujiondoa kutoka kwa muungano wa Ulaya, huku ikiwa haina wabunge wa kutosha bungeni.