Marekani yaitaka China kuikanya Korea Kaskazini

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Rex Tillerson
Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Rex Tillerson

Marekani imeishinikiza China kuongeza jitihada zake katika kuizuia Korea Kaskazini kuendelea na mipango yake ya kinyuklia pamoja na utengezaji wa makombora.

Akizungumza baada ya kukutana na maafisa wakuu wa China, waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Rex Tillerson amesema kuwa Beijing ina jukumu la kidiplomasia kuongeza shinikizo zaidi kwa Pyongyang iwapo ingetaka kupunguza wasiwasi katika eneo hilo.

Katika mkutano huo mjini Washington ambao ulihudhuriwa na waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis bwana Tillerson alisema kuwa China inaunga mkono mpango wa Marekani wa kusitisha mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini pamoja na majaribio ya makombora ya masafa marefu.

Pia ameyataka mataifa yote kuongeza juhudi za kumaliza biashara ya kihalifu ya Korea Kaskazini ambayo anasema inatumika kufadhili mipango yake ya Kinyuklia.