Trump: Ukuta wa Mexico utakuwa na nishati ya jua

Ukuta huo wa Trump utakuwa na paneli za kunasa miale ya jua ili kutengeza kawi ya bei rahisi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ukuta huo wa Trump utakuwa na paneli za kunasa miale ya jua ili kutengeza kawi ya bei rahisi

Rais wa Marekani Donald Trump amewaambia wafuasi wake kwamba pendekezo lake la ukuta katika mpaka na Mexico litakuwa na paneli za kunasa miale ya jua.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika jimbo la Iowa, alisema kuwa paneli hizo za jua zitatoa kawi na kusaidia kulipia ujenzi wa ukuta huo wenye utata.

Alisema kuwa pendekezo hilo ni lake: Ni pendekezo zuri sio, hatahivyo paneli za jua zimeshirikishwa katika muundo wa ukuta huo uliowasilishwa na baadhi ya kampuni.

Wakati wa kampeni yake, bwana Trump aliahidi kujenga ukuta katika mpaka na Mexico ili kuzuia wahamiiaji haramu na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Trump amesema kuwa ukuta wa Mexico utakuwa na nishati ya jua

Amesisitiza kuwa atailazimisha Mexico kulipia ujenzi huo , lakini rais wa taifa hilo Enrique Pena Nieto amepinga mpango huo.

Bwana Trump aliuambia umati uliomshangilia katika mkutano wa kampeni kwamba atatoa pendekezo ambalo hakuna mtu amewahi kulisikia.

''Tunafikiria kitu ambacho ni cha kipekee ,tunazungumzia kuhusu mpaka wa kusini, kuna jua jingi, na joto jingi pia''.

''Tunafikiria kujenga ukuta wa viage vya jua ambao utatengeza kawi na kujilipia. Njia hii Mexico italazimika kulipa fedha kidogo na hilo ni wazo zuri sio?''