Mapambano dhidi ya rushwa kuendelea Tanzania

Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ngazi za juu wa Mapambano dhidi ya Rushwa uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan , amesema kuwa serikali haitarudi nyuma kamwe katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini mpaka hapo vitendo hivyo vitakapokoma.

Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati anafungua Mkutano wa Kimataifa wa ngazi ya Juu wenye lengo la kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya rushwa katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa rais ameeleza kuwa vita ya kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ni kipaumbele cha kwanza katika Serikali ya awamu ya Tano na wale wote wanaowezesha, kunufaika na kuhusika na vitendo hivyo wataendelea kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo nchini humo.

"Kupambana na rushwa ni jambo la msingi na muhimu kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu katika nchi yeyote Duniani," Amesisitiza makamu wa rais Samia Suluhu Hassan.

Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya awamu Tano chini ya Uongozi Shupavu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli inaendelea kukaza kamba katika mapambano dhidi ya rushwa ambayo kwa muda mrefu sasa yamechangia kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Amesema Serikali ya Tanzania inalenga kufikia kipato cha kati na kuimarisha uchumi wa viwanda hadi ifikapo mwaka 2025 hivyo malengo hayo yatafanikiwa haraka iwapo tu vitendo vya rushwa vitakomeshwa katika ngazi zote nchini.

Rushwa ni mbaya na imeharibu sana maisha ya watu na maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo ni lazima ikomeshwe ili jamii iishi maisha mazuri"

Amesema kuwa hakuna nchi yeyote ambayo haijagushwa na misukosuko ya vitendo vya rushwa duniani lakini bara la Afrika limeendelea kuteseka sana na vitendo hivyo kwa miongo kadhaa sasa hivyo jitihada za pamoja zinatakiwa katika kutokomesha vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Waziri wa nchi,ofisi ya rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki amemhakikishia makamu wa rais kuwa wizara yake itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali watumishi wa umma watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwenye maeneo yao ya kazi.

Naye, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia bi Bella Bird amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano za kupambana na vitendo vya rushwa na kusisitiza kuwa Benki hiyo ataendelea kutoa mchango wake wa hali na mali katika kuisaidia Tanzania katika uimarishaji wa mapambano hayo.

Mkutano huo wa Kimataifa wa ngazi ya Juu wenye lengo la kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya Rushwa unaofanyika nchini Tanzania unahudhuriwa na viongozi mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi hiyo wenye uelewa na uzoefu katika mapambano dhidi ya rushwa.