Uingereza ''kuwalinda'' raia wa Ulaya

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, akiwa na mmoja wa viongozi wa Umoja wa Ulaya Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, akiwa na mmoja wa viongozi wa Umoja wa Ulaya

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amewasilisha mipango yake, kuhakikisha haki za raia wa Umoja wa Ulaya nchini humo, baada ya kuondoka katika umoja huo.

Waziri Mkuu May amewaambia viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwamba raia wowote wa umoja huo, ambaye alikuwa Uingereza kwa kipindi cha miaka mitano atapatiwa hadhi mpya ya Uhamiaji, inayomtaja kama ''Mkazi wa Umoja wa Ulaya''.

Hii itawaruhusu kubaki na kuwa na uwezo wa kupata elimu, huduma ya Afya na faida nyingine baada ya Uingereza kujitoa katika umoja huo wa Ulaya.

Waziri mkuuu wa Uingereza pia amesema nchi yake haitaki mkazi yoyote wa sasa wa Umoja wa Ulaya kuondoka nchini humo.

Amesema anatarajia utaratibu huo utakuwa ni wa kukubaliana.

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ahadi hizo zilizotolewa ni mwanzo mzuri, lakini kuna maswali mengi ambayo yanabidi yapatiwe ufumbuzi.