Afisa wa Marekani alitoa ''siri kuu'' kwa ajenti wa China

Afisa mmoja wa kidiplomasia kutoka Marekani amekamatwa na kushtakiwa kwa kutoa nakala za siri kwa ajenti mmoja wa China. Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Afisa mmoja wa kidiplomasia kutoka Marekani amekamatwa na kushtakiwa kwa kutoa nakala za siri kwa ajenti mmoja wa China.

Afisa mmoja wa kidiplomasia kutoka Marekani amekamatwa na kushtakiwa kwa kutoa nakala za siri kwa ajenti mmoja wa China.

Kulingana na hati ya kiapo, Kevin Mallory mwenye umri wa miaka 60 kutoka Virginia anadaiwa kusafiri hadi Shanghai mnamo mwezi Machi na Aprili 2017.

Pia alishindwa kutangaza dola 16,500 fedha taslimu zilizopatikana katika mabegi mawili aliyobeba wakati alipokuwa akisafiri kupitia uwanja wa ndege wa Chicago, kulinga na chombo cha habari cha AP.

Chini ya sheria ya upelelezi atakabiliwa na kifungo cha maisha.

Shirika la kijasusi la FBI nchini Marekani limethibitisha kuwa afisa huyo aliaminiwa sana wakati alipokuwa akiifanyia kazi serikali.

Hatahivyo uaminifu huo uliondolewa baada ya kuacha kufanya kazi na serikali 2012 ambapo alikuwa mshauri wa kibinafsi.

Jarida la Washington Post limesema kuwa kulingana na maafisa wa serikali bwana Mallory aliajiriwa na CIA lakini habari hiyo haikutolewa katika mahakama.

Wakati wa mahojiano ya kujitolea na ajenti wa FBI mnamo mwezi Mei, Bwana Mallory alisema kuwa mtu aliyekutana naye mjini Shanghai alimwambia kwamba alikuwa akilifanyia kazi shirika moja la sayansi mjini Shanghai SASS.

Shirika la ujasusi la FBI limekuwa likiamini kwamba wapelelezi wa China wamekuwa wakilitumia shirika la SASS ili kuficha utambuzi wao kulingana na idara ya haki nchini Marekani.

Hati hiyo ya kiapo pia imeeleza kuhusu habari ambayo bwana Mallory aliandika kwa watu binafsi, akisema lengo lenu ni kupata habari na lengo langu ni kulipwa.