Trump akana kumrekodi aliyekuwa mkurugenzi wa FBI

Donald Trump na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la ujasusi nchini Marekani FBI James Comey
Image caption Donald Trump na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la ujasusi nchini Marekani FBI James Comey

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa hakumrekodi aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la FBI James Comey licha ya kudai hivyo hapo awali.

Alituma ujumbe katika mtandao wake wa Twitter kwamba hakutengeza na wala hana rekodi hizo siku moja baada ya kutakiwa kuwasilisha kanda hizo kwa jopo la Congress.

Bwana Trump alianzisha uvumi wa rekodi hizo katika ujumbe wa Twitter aliochapisha siku moja baada ya kumfuta kazi bwana Comey mnamo mwezi Mei.

Alisema: James Comey uwe na matumaini kwamba sina sina rekodi zozote za sauti yako kuhusu mazungumzo yetu.

Chapisho hilo lilizua madai chungu nzima kwamba bwana Comey alifutwa kazi ili kuzuia uchunguzi kuhusu Urusi kuingilia Uchaguzi wa Marekani mwaka uliopita mbali na ushirikiano wake na kampeni ya rais Donald Trump mjini Moscow.

Licha ya lengo lake kutobainika, ujumbe huo wa Twitter ulisababisha kuajiriwa kwa mtaalam ambaye amechukua uongozi wa uchunguzi wa madai hayo.

Swala hilo linatokana na uchaguzi wa urais wa mwaka jana na ushahidi unaotolewa kwamba wadukuzi wa Urusi walilenga mifumo ya uchaguzi ya Marekani kwa lengo la kumsaidia Donald Trump kushinda kitu ambacho Moscow inakana.