Rais wa zamani wa Botswana Ketumile Masire afariki akiwa na miaka 91

Sir Ketumile Masire

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Sir Ketumile Masire - amechukuliwa na wengi kama mwasisi wa uthabiti wa kisiasa Botswana

Botswana imetangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kufuatia kifo cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Sir Ketumile Masire akiwa na miaka 91.

Sir Ketumile, aliongoza taifa hilo kuanzia 1980 hadi 1998, na amekuwa akisifiwa kwa kuchangia pakubwa katika kuweka msingi imara wa uthabiti wa kisiasa katika taifa hilo, shirika la AFP linasema.

Alishiriki pia katika mikakati ya kufanikisha amani katika mataifa kadha Afrika, ikiwa ni pamoja na kufikisha kikomo vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu nchini Msumbiji.

Botswana ni moja ya nchi tajiri na thabiti zaidi barani Afrika.

Sir Ketumile alichukua uongozi kufuatia kifo cha rais wa kwanza wa Botswana baada ya uhuru Sir Seretse Khama mwaka 1980.

Alitumikia taifa hilo kama waziri wake wa kwanza wa fedha na baadaye kama makamu wa rais kabla ya kuwa rais.

Sir Ketumile alistaafu 1998 baada ya kuongoza taifa hilo katika kipindi cha ukuaji mkubwa wa kiuchumi na usimamizi mwema wa utajiri wa almasi wa Botswana.

Aidha, alishiriki katika kuunga mkono vita dhidi ya serikali ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na kuunga mkono pia harakati za kupigania uhuru katika mataifa mengine ya kanda hiyo.

Kama kiongozi mstaafu, alishiriki katika juhudi za upatanisho kote Afrika, ikiwa ni pamoja na nchini Kenya, Lesotho, Swaziland na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Sir Ketumile alikuwa pia mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Watu Wastahiki ambalo lilichunguza mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.