Trump amteua tajiri Woody Johnson kuwa balozi Uingereza

Woody Johnson Haki miliki ya picha EPA
Image caption Johnson awali alimuunga mkono Jeb Bush

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba atapendekeza rasmi kuteuliwa kwa tajiri mmiliki wa klabu inayocheza ligi ya NFL Woody Johnson kuwa balozi wa Marekani nchini Uingereza.

Ni mmiliki wa klabu ya New York Jets ambayo haijakuwa ikifanya vyema Ligi ya Soka ya Taifa (NFL).

Bilionea huyo ni mrithi mtarajiwa wa kampuni kubwa ya dawa ya Johnson & Johnson na amefahamiaka na Bw Trump kwa miaka mingi.

Hata hivyo, Bw Johnson, 70, ambaye alichangia sana juhudi za chama cha Republican kuchangisha pesa, awali aliunga mkono mpinzani wa Trump katika mchujo wa chama hicho Jeb Bush.

Amechangia mamilioni ya dola katika mipango na juhudi za chama cha Republican.

Atahitaji kuidhinishwa na bunge la Seneti kabla ya kuchukua rasmi majukumu.

Bw Trump alizua wazo la kumteua kwua balozi mwezi Januari, mkesha wa kuapishwa kwake kuwa rais.

Wadhifa wa balozi wa Marekani nchini Uingereza umekuwa ukitazamwa na wengi kama wadhifa mkuu katika diplomasia, na sana huwa unapewa watu wanaochanga zaidi pesa katika kampeni au washirika wa karibu kisiasa wa utawala.

Waziri Mkuu wa Theresa May amekaribisha uteuzi huo, shirika la habari la Reuters limeripoti.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii