Saudia yatibua shambulio la kigaidi lililolenga msikiti wa Grand Mosque Mecca

Msikiti wa Grand Mosque ulio na al kaaba mjini Mecca Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Msikiti wa Grand Mosque ulio na al kaaba mjini Mecca

Wizara ya mambo ya ndani nchini Saudia inasema maafisa wa usalama wamesambaratisha njama ya shambulizi la kigaidi lililolenga msikiti wa Grand Mosque mjini Mecca.

Msemaji wa polisi anasema mshukiwa wa shambulizi hilo alifumaniwa kwenye jengo la makaazi ambapo alijilipua na kubomoa jengo hilo, baada ya ufyatulianaji risasi na polisi kwa muda mfupi.

Watu 11, wakiwemo mahujaji 6 wa kigeni na maafisa 5 wa usalama walijeruhiwa.

Wizara hiyo aidha inasema watu watano akiwemo mwanamke mmoja walitiwa mbaroni katika maeneo yanayokisiwa kuwa maficho ya magaidi katika mji wa Mecca na Jeddah.

.Jengo hilo lilianguka na kuwajeruhi watu 11 ikiwemo maafisa wa polisi .

Washukiwa wengine watano wamekamatwa, maafisa wanasema.

Maafisa wa Saudia hawakutoa maelezo zaidi kuhusu kutibuliwa kwa shambulio hilo.

Saudia katika miaka ya hivi karibuni imekabiliwa na mashambulio mabaya ya mabomu mengi yakitekelezwa na wapiganaji wa Islamic State.

Mashambulio mengi yamelenga watu wa madhehebu ya shia walio wachache na vikosi vya usalama.

Manmo mwezi Julai 2016, maafisa wanne wa usalama waliuawa katika shambulio la kigaidi karibu na msikiti wa mtume Mohammed mjini Medina.

Saudia ni mwanachama wa muungano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani yanayokabiliana na Islamic State pamoja na makundi mengine ya Kijihadi nchini Syria na Iraq.