Hatua ya kuupa mtaa jina la Wanyama yazua utata Tanzania

Jina la mtaa uliokuwa katika Barabara iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Viwandani ulipewa jina la Wanyama Haki miliki ya picha Victor Wanyama/Instagram
Image caption Jina la mtaa uliokuwa katika Barabara iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Viwandani ulipewa jina la Wanyama

Utata umegubika hatua ya meya wa Manispaa ya Ubongo Boniface Jacob, kumtunuku mtaa, Kiungo wa Tottenham ya England Victor Wanyama ambaye ni raia wa Kenya.

Jina la mtaa uliokuwa katika Barabara iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Viwandani ulipewa jina la Wanyama, baada ya mchezaji huyo ambaye amekuwa ziarani Tanzania kuhudhuria mashindano ya Kombe la Ndondo katika Uwanja wa Kinesi Ubungo Shekilango jijini Dar es Salaam Jumamosi jioni.

Lakini leo, Kitengo Cha Habari na Uhusiano Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kimetoa taarifa na kusema hatua hiyo ya Meya Jacob haikufuata utaratibu uliopo kisheria.

"Majina ya mitaa hupendekezwa na kamati za mitaa husika kisha hupelekwa kwenye vikao vya WDC vya kata halafu maamuzi ya WDC hupelekwa kwa Mkurugenzi kwa ajili ya kuingizwa kwenye kikao Cha kamati ya Fedha na uongozi, Baraza la Madiwani, halafu DCC, RCC na Kisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na baadaye kwa Mchapaji mkuu wa serikali na mwisho hutokea kwenye Tangazo la serikali GN," taarifa hiyo iliyotumwa wka vyombo vya habari imesema.

"Na hapo ndipo mtaa hujulikana huo ni mtaa fulani. Taratibu za kubadili pia lazima zifuate hatua hizo muhimu."

"Kilichofanyika ni kinyume na utaratibu wa kisheria".

Picha moja iliyosambazwa mtandaoni Jumapili ilionesha mtu ambaye jina lake halifahamika mara moja akiwa amebeba bango la kuashiria jina la barabara hiyo ambalo lilikuwa limewekwa jana.

Wanyama awali alikuwa ameonesha kufurahishwa sana na hatua ya manispaa hiyo kuupa mtaa jina lake.

Kwenye video aliyoipakia katika ukurasa wake wa Instagram aliandika: "Nitoe Shukrani zangu za dhati kwa Mayor na wakaazi wote wa Manispaa ya Ubungo kwa kunikaribisha na kulipatia jina langu barabara ya mtaa wa NHC.

Naahidi kurudi tena na Ahsanteni sana kwa ukarimu na makaribisho mlionipa. Asante Tanzania."