Reli mpya ya kisasa itaifaa Kenya?

Reli ya kisasa ya SGR nchini Kenya iliyozinduliwa ilikuwa ni matokeo ya maafikiano kati ya Serikali ya Kenya na China ambapo China ilifadhili asilimia 80 na Kenya ikafadhili asilimia 20 iliyobaki.
Image caption Reli ya kisasa ya SGR nchini Kenya iliyozinduliwa ilikuwa ni matokeo ya maafikiano kati ya Serikali ya Kenya na China ambapo China ilifadhili asilimia 80 na Kenya ikafadhili asilimia 20 iliyobaki.

Kenya ilizindua reli yake ya kisasa mwanzoni mwa mwezi huu ambayo ndiyo ya kwanza kujengwa katika taifa hilo katika taifa hilo katika kipindi cha karne moja.

Reli hiyo inatoka Mombasa hadi Nairobi. Hata hivyo, ingawa imesifiwa sana na serikali, kunao wanaotilia shaka uwezo wake wa kulipia gharama ya ujenzi.

Reli hiyo iligharimu $5.6m kwa kila kilomita, kiwango ambacho ni mara tatu zaidi ya kiwango cha wastani cha gharama kimataifa. Aidha, gharama hiyo ni mara nne zaidi ya makadirio ya kwanza ya gharama.

Hivyo basi, si ajabu kwamba baadhi ya Wakenya, sana katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakishangaa ni kwa nini mradi huo wa ujenzi uligharimu kiasi kikubwa hivyo cha pesa.

Reli hiyo mpya ya Kenya ya urefu wa 472km (maili 293) ndio mradi mkubwa sana wa miundo mbinu uliotekelezwa na Kenya tangu uhuru mwaka 1963. Njia hiyo ya treni imejengwa kwa kufuata viwango vya kisasa na inafuata njia ya reli ya zamani iliyojengwa wakati wa ukoloni.

Ingawa wengi wanakubali kwamba Kenya inahitaji miundo mbinu zaidi, si wote wanaokubali kwamba mradi huo ulikuwa mwafaka zaidi.

Wengi wamekuwa wakilinganisha gharama ya ujenzi wa reli hiyo na gharama ya reli ya urefu wa 756km kutoka Addis Ababa, nchini Ethiopia hadi Djibouti, reli ambayo ilizinduliwa mwaka jana.

Reli zote mbili zinafuata viwango vya kisasa (SGR) na zilifadhiliwa kwa mikopo kutoka China, lakini gharama ya reli ya Ethiopia ilikuwa jumla ya $3.4bn (£2.6bn) nayo ya Kenya iligharimu $3.2bn.

Reli ya Ethiopia ni ndefu kuliko kwa Kenya kwa 250km na treni zake zitatumia umeme, hivyo inafaa kuwa ghali kiasi. Treni zitakazotumia reli ya Kenya zitatumia dizeli.

Image caption Awamu ya mwisho 2(b) itakayounganisha Naivasha – Kisumu – Malaba itagharimu dola 3.5 bilioni.

Serikali ya Kenya imejitetea kwamba gharama ya juu ya mradi huo ilitokana na kuwepo na milima na mabonde ambayo halilazimisha kujengwa kwa madaraja mengi na njia za chini kwa chini. Aidha, serikali imesema pesa za kulipa fidia wamiliki wa ardhi ambayo ilihitajika kwa ujenzi wa mradi huyo zilichangia ongezeko la gharama. Isitoshe, serikali ilisema reli hiyo ilihitaji kujengwa kwa kiwango cha juu kwa sababu itakuwa ikitumiwa kusafirisha kiasi kikubwa cha mizigo kuliko reli hiyo ya Ethiopia.

Kwa Picha: Kenya yapokea mabehewa mapya ya treni

Kwa hivyo, serikali inasema si haki kulinganisha miradi hiyo miwili.

Takriban asilimia 80 ya pesa zilizotumiwa kujenga reli hiyo zilipatikana kupitia mikopo kutoka China.

Mikopo hiyo ndiyo ya juu zaidi kwa Kenya, na ni karibu 6% ya jumla ya mapato ya taifa la Kenya kwa mwaka (GDP), ambayo ni kiashiria cha shughuli za kiuchumi katika taifa, pamoja na huduma na bidhaa zote zinazozalishwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Hata kabla ya Kenya kuanza ujenzi huo, washauri wa serikali kutoka Canadian Pacific Consulting Services (CPSC) walitilia shaka manufaa ya mradi huo kiuchumi mwaka 2009.

Washauri hao walisema manufaa ya ujenzi wa reli hiyo yatakuwa madogo. Mradi huo, washauri hao walisema, ungekuwa wa "gharama kubwa sana" hata kwa kutumia makadirio ya juu zaidi ya kutumiwa sana kwa uchukuzi na mapato yenyewe.

Lakini waziri wa uchukuzi James Macharia alisema serikali ya Kenya inatarajia reli hiyo itaimarisha GDP kwa asilimia 1.5%, na kuwezesha mikopo hiyo kutoka China "kujilipa kwa miaka minne hivi".

Makadirio hayo yake yanaenda kinyume na wasiwasi kwamba Kenya hivi karibuni huenda ikashindwa kulipa mikopo hiyo kutokana na mikopo mingine ambayo tayari Kenya imekopa.

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kuchukua mikopo kwa wingi kumesababisha mikopo ambayo Kenya inadaiwa kuwa zaidi ya nusu ya GDP, lakini mapato hayajakua kwa kiwango hicho.

Sehemu kubwa ya mapato kutoka kwa reli hiyo mpya inatarajiwa kutoka kwa uchukuzi wa mizigo. Kwa sasa, ni 5% pekee ya mizigo husafirishwa kwa kutumia reli ya zamani na 95% husafirishwa kwa kutumia barabara. Lakini Shirika la Reli la Kenya linalenga kuimarisha kiasi hicho hadi 40% kufikia 2025 kutokana na reli hiyo mpya.

Kuna uwezekano kwamba kutapitishwa sheria mpya la kulazimisha aina fulani ya bidhaa kusafirishwa kwa reli kuhakikisha mizigo mingi inasafirishwa kwa kutumia reli.

________________________________________

Kwa muhtasari:

  • Gharama $3.2bn (£2.5bn)
  • Ufadhili wa ujenzi wa reli hiyo ya 472km (maili 293) ulitoka China
  • Ilichukua miaka mitatu unuzu kujenga reli hiyo
  • Reli hiyo inatarajiwa mwishowe kuendelezwa na kuunganisha Sudan Kusini, maeneo ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Burundi na Ethiopia na Bahari ya Hindi
  • Imepunguza muda unaotumiwa kusafiri kati ya Mombasa na Nairobi hadi saa nne unusu, ukilinganisha na hadi saa nane kwa kutumia basi au saa 12 ukitumia reli ya zamani awali
  • Tiketi ya kawaida inagharimu shilingi 700 za Kenya ($7), ambayo ni nafuu ukilinganisha na nauli ya basi. Tiketi mabehewa ya kifahari ni $30

________________________________________

Reli hiyo pia inakabiliwa na ushindani katika kanda. Tanzania na Kenya zinashindana kuwa njia ya kupitishia bidhaa kutoka na kuelekea Uganda, Rwanda na Burundi.

Utafiti wa Benki ya Dunia wa mwaka 2013 ulitabiri kwamba mizigo ambayo itakuwa ikisafirishwa kwa reli kote Afrika Mashariki ingeongezeka na kufikia takriban tani 14.4 milioni kufikia mwaka 2030.

Utafiti huo pia ulitabiri kwamba uwekezaji katika reli mpya ya kisasa ungekuwa na maana iwapo ungefanikiwa kuvutia mizigo zaidi kusafirishwa kwa reli na inafaa kuongezeka kwa tani milioni 20-55 milioni kwa mwaka.

Ili kufikia kiwango hicho, reli itahitajika kutumiwa kusafirisha mizigo yote inayofika bandari ya Mombasa - na zaidi.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya, bandari ya Mombasa ilisafirisha mizigo tani 26 milioni mwaka 2015.

Licha ya changamoto hizi, hakuna shaka kwamba reli hiyo mpya itakuwa na manufaa ya muda mrefu ya kiuchumi.

Abiria watasafiri haraka na kwa gharama nafuu na kuongezeka wka mizigo itakayosafirishwa kwa treni kutasaidia kupunguza mizigo inayosafirishwa kwa malori na hivyo kupunguza kasi ya kuharibika kwa barabara.

Gharama ya kusafirisha mizigo kwa kila kilomita katika kanda hii huwa 50% zaidi ukilinganisha na Marekani na Ulaya, hivyo kuwepo kwa njia nafuu ya kusafirisha mizigo kwa treni kutasaidia sana wafanyabiashara.

Kuna nafasi nyingi za kazi ambazo zitabuniwa moja kwa moja na mradi huu - nafasi za ujenzi, ukarabati na utunzaji wa reli. Kutakuwa pia na nafasi za wahudumu wa treni na wengine vituo vya treni. Miji ambayo treni zitakuwa zikisimama pia itashuhudia kuimarika kwa biashara.

Kenya inaongoza kwa uuzaji nje wa bidhaa Afrika Mashariki, na reli hiyo mpya itasaidia sana kuunganisha Kenya na majirani zake kwa reli, na kuifanya rahisi kwa mataifa ya kanda kuuza bidhaa nje.

Bila shaka mradi huu utakuwa ishara ya maendeleo, lakini ndipo kupata manufaa kamili, itategemea kiasi cha mizigo itakayosafirishwa kupitia reli hiyo pamoja na abiria pia watakaoitumia.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii