BBC Swahili yasherehekea miaka 60 ya utangazaji

Alois Ngosso, mmoja wa watangazaji wa BBC Swahili miaka ya sitini
Image caption Alois Ngosso, mmoja wa watangazaji wa BBC Swahili miaka ya sitini

Idhaa ya Kiswahili ya BBC ilizinduliwa mnamo 27 Juni 1957 na itakuwa inasherehekea kutimiza Miaka Sitini wiki hii. Kutakuwa na makala na taarifa maalum wiki yote kuadhimisha hatua hii muhimu.

Vipindi maalum vya maadhimisho vya AMKA na BBC (redio) na Dira ya Dunia (TV na redio) vitaangazia hatua zilizopigwa na BBC Swahili katika historia yake.

Taarifa zitaangazia ukuaji wa Kiswahili katika tasnia ya utangazaji, mchango wake katika ukuaji wa demokrasia na jinsi BBC Swahili imechangia kubadili maisha ya wasikilizaji.

Idhaa hii pia itaangazia burudani kutoka kanda ya Afrika Mashariki na Kati - hasa Midundo ya nyimbo za Kiswahili ilivyobadilika.

Watangazaji wa zamani wa BBC pia watakuwa wakichipuka na kutafakari pamoja na kueleza jinsi hali ilivyobadilika tangu kupeperushwa hewani kwa matanagzao ya kwanza London.

Pamoja na haya, kutakuwepo pia na mjadala wa kipekee utakaofanyika Dar es Salaam Jumanne 27 Juni, tarehe kamili ambayo matangazo ya kwanza ya Kiswahili yalikwenda hewani miaka sitini iliyopita.

Mada ya mjadala huo ni: Kiswahili Changu. Mdahalo huu utaangazia jinsi lugha hii inayotumiwa na watu wengi Afrika Mashariki imebadilika, pamoja na lahaja zake mbalimbali na jinsi watu kutoka nje wanavyokikumbatia Kiswahili. Kutakuwa na jopo la wataalamu wakiwakilisha wasikilizaji wa BBC Swahili pamoja na wenyeji.

Kutakuwa pia na makala maalum mtandaoni kwa ajili ya wazungumzaji wa Kiswahili kote duniani, kuwawezesha kuzipata kwa urahisi. Kutakuwa na video za ucheshi kuhusu waandishi na watangazaji wa BBC Swahili, makala ya kulinganisha teknolojia ya uanahabari ilivyobadilika kupitia mtangazaji wa zamani wa idhaa na mtangazaji aliyejiunga na idhaa majuzi.

Image caption Salim Kikeke mwaka 2008

Kadhalika, kutakuwa na shabiki wa mtandaoni wa BBC ambaye ataeleza mengi kumhusu na pia kujumuika na waandishi na watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC. Aidha, utapata pia makala ya kina kuhusu historia, hatua muhimu zilizopigwa na idhaa hii na pia mkusanyiko wa picha zinazosimulia mambo yalivyobadilika - ambazo huwezi kuzipata kwingine.

Kipindi hicho cha miaka sitini BBC Swahili imekua kwa mapana na marefu, kutoka kuwa kituo cha redio pekee hadi kuwa na runinga na pia majukwaa mtandaoni ambapo kila siku hupeperusha taarifa za kina kutoka kila pembe ya dunia kwa mamilioni ya wasikilizaji, wasomaji na watazamaji.

Image caption Caroline Karobia

Mhariri wa BBC Swahili Caroline Karobia anasema, "Tunajivunia sana historia yetu ya utangazaji na tunatumai kwamba tutaweza kuendelea kuimarika na kuwahudumia wasikilizaji na watazamaji wetu wka miaka mingi ijayo. Tuna furaha sana kutokana na fursa zinazoletwa na teknolojia mpya kutuwezesha kufikia watu wengi zaidi na kwa karibu zaidi."

Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea BBCSwahili.com

Mada zinazohusiana