Trump afurahia uamuzi wa mahakama kuikubalia marufuku dhidi ya wahamiaji Marekani

Los Angeles International 4 Februari 2017 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Marufuku ya awali iliyotangazwa Januari ilisababisha maandamano viwanja vya ndege Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amefurahia uamuzi wa Mahakama ya Juu nchini humo kuruhusu baadhi ya vifungu vya marufuku yake ya usafiri viendelee kutumika.

Kiongozi huyo amesema uamuzi huo ni "ushindi wa usalama wa taifa".

Mahakama hiyo ya juu zaidi ilikubali ombi la White House la kuruhusu sehemu ya marufuku yake dhidi ya wahamiaji kuanza kutekelezwa.

Majaji wamesema watatoa uamuzi kamili Oktoba kuhusu iwapo marufuku hiyo inafaa kudumishwa au kufutiliwa mbali.

Bw Trump anataka kuwepo na marufuku ya siku 90 kzuuia watu kutoka mataifa sita yenye Waislamu wengi wasiingie Marekani, na siku 120 dhidi ya wakimbizi.

Rais huyo amesema uamuzi wa mahakama sasa unaukubalia utawala wake kuzuia wageni kutoka Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen, nchi ambazo anasema zina hatari kubwa sana ya ugaidi.

"Kama rais siwezi kuruhusu watu ambao wanataka kutudhuru waingie nchini," ameongeza.

Bw Trump tayari amesema marufuku hiyo itaanza kutekelezwa katika kipindi cha saa 72 baada ya uamuzi huo wa mahakama.

Uamuzi wa mahakama unasemaje?

Mahakama ya Juu imesema amri ya rais iliyotangaza amrufuku hiyo haiwezi kutekelezwa dhidi ya raia wa nje ambao wana jamaa au uhusiano na mtu au shirika lililopo Marekani.

Hata hivyo, raia wengine wote wa nje ya nchi hiyo wanaweza kuathiriwa na marufuku hiyo.

Mahakama imesema pia kwamba itaruhusu kuanza kutekelezwa kwa marufuku ya siku 120 ya kuzuia wakimbizi kuingia nchini humo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii