Theresa May aahidi usawa kwa raia wa Ulaya

May asema hakuna haki ya mtu itakayopotea
Image caption May asema hakuna haki ya mtu itakayopotea

Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May ameelezea mpango wake wa kuwataka raia milioni tatu wa mataifa ya umoja wa Ulaya wanaoishi Uingereza kusalia nchini humo hata baada ya nchi yake kujitoa ndani ya umoja wa Ulaya.

Kauli yake inakuja baada ya hali ya sintofahamu juu ya hatma ya watu hao.

Bi May amesema watu hao watakuwa na haki sawa na raia wa Uingereza kama vile kupata huduma za matibabu, elimu na mafao mengine muhimu.

Chini ya mapendekezo hayo serikali ya Uingereza itafanya kila iwezalo kufanikisha mchakato huo kwa raia wa mataifa ya EU ambao wameishi Uingereza kwa zaidi ya miaka mitano.

Image caption Zaidi ya Waingereza milioni 17 walipiga kura ya kuondoka ndani ya umoja wa Ulaya

Mpatanishi kuu wa EU juu ya brexit, Michel Barnier, amesema lengo lake juu ya masuala ya haki kwa raia wa mataifa wanachama wa EU ni kuhakikisha wanapata haki kwa mujibu wa sheria za umoja huo, na kuongeza kuwa Uingereza inastahili kutoa muelekeo na hakikisho zaidi kuhusu msimamo wake juu ya suala hilo.