Miaka 60 ya BBC Swahili: Ni nani mwingine ametimiza miaka 60?

BBC Swahili inaadhimisha miaka 60 katika tasnia ya uanahabari. Tunaangalia ni nani au nini ambacho pia kinasherehekea hatua hii muhimu?

1. Alhaji Aliko Dangote - Nigeria

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Dangote alizaliwa Kano, katika familia maarufu ya wafanyabiashara, Aprili 10, 1957.

Ni raia wa Nigeria aliyetajwa na jarida la Forbes kama mtu tajiri zaidi Afrika na pia ni kati ya watu 100 matajiri zaidi duniani. Mali yake inakadiiriwa kuwa zaidi ya bilioni 4.5 dola za Marekani.

Dangote alizaliwa Kano, katika familia maarufu ya wafanyabiashara, Aprili 10, 1957.

Yeye ni mjukuu wa Alhaji Alhassan Dantata, mmoja wa Waafrika waliokuwa matajiri zaidi wakati wake. Dantata alifariki dunia 1955.

2. Ghana

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ghana iliadhimisha miaka 60 ya kujitawala, Machi 6, 2017.

Machi 6, 2017 Ghana iliadhimisha miaka 60 ya kujitawala. Nchi hii ilitawaliwa na Uingereza kwa miaka 113.

Nchi hii, ambayo zamani, ilijulikana kama Gold Coast ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara kujipatia uhuru na Rais wake wa kwanza alikuwa Dkt. Kwame Nkrumah

3. Shule ya wasichana ya Ngara, Nairobi

Image caption Shule ya sekondari ya Ngara jijini Nairobi ilifunguliwa Januari 1957 kama shule ya sekondari ya mseto kwa wanafunzi wenye asili ya kihindi

Ilifunguliwa Januari 1957 kama shule ya sekondari ya mseto kwa wanafunzi wenye asili ya kihindi.

Mkuu wa kwanza wa shule hiyo alikuwa Bw Waller. Miaka mitano baadaye, mwaka wa 1962, wavulana walihamia eneo la South B ambako walianzisha shule ambayo kwa sasa ni shule ya sekondari ya Highway.

Mwaka uliofuata, 1963, shule hiyo ambayo sasa ilikuwa shule ya wasichana, ilipokea Mwalimu mkuu wa kwanza wa kike, Bi Serah Joseph ambaye alihudumia shule kwa mwaka mmoja tu.

Alibadilishwa na Bi Reina D'Souza mwaka wa 1964.

Ni mwaka huo ambao Tume ya Ominde ilitupilia mbali mfumo wa elimu katika shule za Kenya uliobagua wanafunzi kwa misingi ya rangi, na shule ya sekondari ya Ngara ikafunguliwa kwa wanafunzi kutoka jamii zote.

4. Mnara wa saa wa City Hall, Nairobi

Kufuatia kuopngezeka kwa mahitaji ya wakazi na baraza la jiji, iliamuliwa kuwa baraza hilo lilihitaji makazi zaidi ya kutoa huduma kwa wakazi.

Image caption Mnara wa saa wa City Hall ulikuwa jengo refu zaidi jijini Nairobi mwaka wa 1957.

Ujenzi wa makao makuu mapya ulianza mwaka wa 1950 na kukamilika mwaka wa 1957.

Jumba hilo lilijengwa pamoja na mnara wa saa wa futi 165 wa City Hall na kufunguliwa rasmi mwaka wa 1957. Ulikuwa jengo refu zaidi jijini Nairobi mwaka wa 1957.

5. Kifo cha Dedan Kimathi

Image caption Sanamu ya futi saba iliwekwa wakati wa utawala wa Rais Kibaki katika barabara ya Kimathi kwa heshima kwa Kimathi, aliyenyongwa na wakoloni 1957.

Dedan Kimathi Waciuri alizaliwa Kimathi wa Waciuri, na alikuwa kiongozi wa kundi la Mau Mau, kikundi ambacho kilipigana dhidi ya utawala wa ukoloni wa Uingereza nchini Kenya miaka ya 1950.

Ni miaka 60 tangu Kimathi kuuawa. Alikamatwa Karunaini, Tetu, jimbo la Nyeri mwaka wa 1956 na askari wawili waliojulikana tu kama Ndirangu na Njogu.

Kimathi aliuawa kwa kunyongwa na wakoloni tarehe 18 Februari, 1957.

Miaka kumi iliyopita, Rais Mwai Kibaki alizindua sanamu ya futi saba kama heshima kwa Kimathi, katika makutano ya barabara za Kimathi na Mama Ngina jijini Nairobi.

6. Express FC - Uganda.

Klabu ya Express FC inajulikana na mashabiki wake kama Red Eagles na pia ilijulikana kama Express Sports Club.

Ilikuwa klabu ya kwanza kuu ya soka nchini Uganda, baada ya kuanzishwa mwezi Oktoba 1957 na mameneja wa Magazeti ya Uganda Express.

Wachezaji wa Red Eagles walikuwa wa kwanza nchini Uganda kutumia viatu rasmi vya soka uwanjani.

Kwa jumla Express FC imeshinda mataji sita ya ligi .

7. Umoja wa Ulaya, EU

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Machi 25, 1957, Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya (EEC) ambayo sasa ni EU ilianzishwa

Machi 2017, iliadhimisha miaka 60 ya kuwepo kwa Umoja wa Ulaya, ambayo ni jumuiya kubwa duniani ya kisiasa na kiuchumi.

Machi 25, 1957, Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya (EEC) ambayo sasa ni EU ilianzishwa wakati wawakilishi kutoka Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Luxemburg na Uholanzi walitia saini Mkataba wa Roma.

Nchi 28 ni wanachama wake na wanashirikiana kila kitu ikiwemo biashara, kukabiliana na ugaidi na masuala ya utalii.

Mwaka 2012, EU ilipokea tuzo ya Amani ya Nobel kwa kuendeleza amani, demokrasia, upatanisho na haki za binadamu barani Ulaya.