Wapiga kura 88,000 wafu waondolewa kwenye sajili Kenya

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya Bw. Chebukati
Maelezo ya picha,

Wapiga kura wataweza kuhakiki maelezo yao kwa simu kuanzia Alhamisi 29 Juni

Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC) imeyaondoa majina ya watu 88,602 ambao walikuwa wamefariki dunia kutoka kwenye sajili ya wapiga kura, taarifa kutoka kwa tume hiyo imesema.

Tume hiyo ilikuwa imefahamishwa kwamba kuna jumla ya watu 92,277 walioaga dunia waliokuwa kwenye sajili baada ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya KPMG, lakini kampuni hiyo baadaye ilibadilisha idadi hiyo hadi 88,602 baada ya kubainika kwamba huenda taarifa kuhusu waliofariki zilipigwa mara zaidi ya moja.

"Tunafahamu kuwa sajili ya wapigaji kura haiwezi kosa majina kadhaa ya wafu. Lakini tunaamini kuwa teknolojia ya KIEMS itathibitisha kwa uhakika siku ya uchaguzi na hakutakuwa na nafasi ya utundu," Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati amesema.

Orodha ya wapigaji kura iliyoidhinishwa kutumiwa katika uchaguzi mkuu mwaka huu ina jumla ya wapigaji kura 19,611,423, wakiwemo watu 4,393 walio ng'ambo katika nchi 5 na watu 5,528 waliosajiliwa katika jela 118 nchini Kenya.

Idadi ya wapigaji kura imneongezeka kwa asilimia 36 ukilinganisha na wapiga kura 5,222,642 waliokuwepo mwaka 2013.

Tume imesema kuwa orodha kamili ya wapiga kura itapakiwa mtandaoni na watu wanaweza kuchunguza iwapo majina yao yamo kwenye sajili kwa kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu kuanzia Alhamisi 29 Juni hadi siku ya uchaguzi.

Asilimia 53 ya wapiga kura mwaka huu ni wanaume na asilimia 47 ni wakawake. Kiwango cha wanawake kwenye sajili kimepungua kwa asilimia 2 mwaka huu.

Asilimia 51 ya wapiga krua waliosajiliwa wana umri wa kati ya miaka 18 na 35.

Kutakuwa na vituo 40,883 vya kupigia kura ambavyo kila kimoja kina chini ya wapiga kura 700.