Trump aanza kutafuta pesa za kampeni ya 2020

Protests outside Trump hotel Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji walikusanyika nje ya hoteli hiyo ya Trump

Rais wa Marekani Donald Trump ameandaa hafla ya kuchangisha pesa kwa ajili ya kampeni za urais za mwaka 2020.

Hafla hiyo iliandaliwa katika hoteli moja mjini Washington.

Waandamanaji hata hivyo walimkaripia rais wakisema kwa sauti "Aibu!" alipowasili kuhudhuria hafla hiyo.

Kwenye hafla hiyo, kila aliyehudhuria alikuwa analipa $35,000 (£27,000).

Wengi wa waandamanaji walikuwa hawajaridhishwa na mpango wa bima ya afya wa chama cha Republican, na walikuwa na mabango yenye ujumbe "Bima ya afya, na wala si kupunguzwa kwa kodi."

Hali kwamba mchango huo ulifanyika katika hoteli ya Trump International imeibua tena wasiwasi kuhusu muingiliano wa maslahi kati ya majukumu ya Bw Trump kama rais na biashara zake.

Richard Painter, ambaye alihudumu katika ikulu ya White House kama mwanasheria aliyehusika na masuala ya maadili wakati wa utawala wa rais wa zamani George W Bush, amesema haikubaliki kwa rais kuonekana akifaidi kifedha kutoka kwa hafla ya aina hiyo.

Familia ya Donald Trump: Wake na watoto

Wasifu wa Trump, rais wa Marekani

Amesema rais huyo angechagua hoteli nyingine na wala si moja ya hoteli zake.

Lakini Kathleen Clark, profesa wa masuala ya uanasheria anayeangazia fani ya maadili katika Chuo Kikuu cha Washington mjini St. Louis, aliambia USA Today, kwamba Trump hakuvunja sheria zozote.

Haijabainika bado iwapo hoteli hiyo ililipwa kuwa mwenyeji wa hafla hiyo.

Maafisa wa kamati ya taifa ya chama cha Republican walitarajia kuchangisha takriban $10m, kulikuwa na nafasi 300 zilizokuwa zinauzwa.

Pesa zote hata hivyo hazitatumiwa kwa kampeni ya Trump 2020 - kuna nyingine zitatumiwa na chama cha Republican.

Ni jambo lisilo la kawaida kwa rais kuanza kuchangisha pesa za kutetea kuchaguliwa tena mapema hivyo muhula wake wa kwanza.

Trump amehudumu kama rais kwa miezi mitano pekee.

"Bila shaka atapigania kuchaguliwa tena,2 msemaji wa White House Sarah Huckabee Sanders aliambia wanahabari Jumatano.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii