'Malkia wa Rumba' Mbilia Bel atua Nairobi kueneza amani

Mbilia Bel alivuma sana kwa nyimbo zake kama vile Nakei Nairobi
Image caption Mbilia Bel alivuma sana kwa nyimbo zake kama vile Nakei Nairobi

Mwimbaji mashuhuri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mbilia Bel amewahakikishia mashabiki wake wa Kenya kwamba atawatumbuiza vilivyo Ijumaa wiki hii atakapokua jukwaani jijini Nairobi.

Mbilia Bel aliwasili Nairobi wiki hii kwa mwaliko wa Pamela Olet wa kampuni ya Melamani Productions, lengo kubwa la ziara yake ya wiki mbili nchini Kenya ni kueneza amani na kutumbuiza mashabiki wake na nyimbo zake zilizotia fora kama vile Nakei Nairobi, Eswi Yo Wapi na Nadina alizoimba na marehemu Tabu Ley aliyekuwa kiongozi wa Afrisa International.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC akiwa safarini kuelekea Nairobi kutoka Congo Brazzaville, Mbilia alisema amefurahi kurudi Nairobi baada ya miaka 16.

"Napenda sana mashabiki wangu wa Kenya kwa sababu wananionyesha upendo na wanafurahia nyimbo zangu,'' alisema Mbilia Bel ambaye sasa ana umri wa miaka 58 lakini bado ni mrembo tu sana utadhani ana umri wa miaka ishirini hapo.

Nini siri yake ya urembo? "Mimi nala sana maharage na hilo limenisaidia kuwa nilivyo najua wanaume wa Nairobi watanimezea mate lakini hapa nimekuja kwa kazi,'' alisema Mbilia Bel kwa utani.

Anatarajiwa kuzuru wafungwa wa jela ya wanawake ya Langata mjini Nairobi Alhamisi wiki hii.

Albamu yake ya mwisho, Signature, ni kuhusu maisha yake yanayoangazia uzuri wake na ubaya.

Anamsifu sana Tabu Ley kwa kukuuza kipaji chake akiwa mnenguaji akapanda ngazi na akawa mwimbaji.

Gwiji Tabu Ley hakukuza tu kipaji cha Mbilia Bel bali alimpenda pia na hatimaye Mbilia akawa mpenzi wake na kumzalia mtoto aitwaye Melody.

Aliacha bendi ya Tabu Ley mwaka wa 1987 pale penzi lake na Tabu Ley lilipoanza kuyumbayumba mwimbaji mwingine hodari Faya Tessa alipojiunga na bendi hiyo.

Mbilia hakufurahia jinsi Faya Tess alimnasa Tabu Ley wakawa na chuki kupita kiasi wote wawili kila mmoja wao akitaka kuonekana ndiye anapendwa zaidi ya mwenzake.

Baada ya kutumbuiza Nairobi, Mbilia ataelekea Kisumu kuchangamsha mashabiki wake wengi huko Julai tarehe saba.

Mada zinazohusiana