Muungano wa majeshi ya Marekani yaukomboa mji wa Mosul

Wanajeshi wanaoungwa mkono na Marekani waukomboa mji wa Mosul kutoka kwa mikono ya IS Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wanaoungwa mkono na Marekani waukomboa mji wa Mosul kutoka kwa mikono ya IS

Muungano wa wanajeshi wa Iraq wanaoongozwa na Marekani katika vita dhidi ya wanamgambo wa Islamic State mjini Mosul, unasema kuwa umepata ushindi mkubwa na kuuteka msikiti mkubwa wa Mosul uliolipuliwa.

Msemaji wa muungano huo Kanali Ryan Dillon, anasema kuwa, ingawa mji wa kale wa Mosul, unasalia kuwa mapigano magumu na makali, unatarajia kuchukua siku au hata majuma kadhaa, kwa mapigano kumalizika.

Awali, serikali ya Iraqi iliisifu hatua ya kuchukua udhibiti wa msikiti maarufu wa Nuri mjini Mosul, na kusema kuwa huo sasa umebadilisha sura ya mapigano hayo dhidi ya Wanajihadi hao.

Katika nchi jirani ya Syria, wanajeshi wanaoungwa mkono na Marekani, wanasemekana kuzingira kabisa ngome ya IS huko Raqqa.

Kwa kutumia neno linalotumia na Wanajihad hao, waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alisema kuwa utekaji wa msikiti huo uliadhimisha mwisho wa Jimbo la Daesh.

''Hatutasalimu amri, majeshi yetu jasiri yatatupatia ushindi'', ,aliongezea.Tutaendelea kukabiliana na Daesh hadi kila mmoja wao atakapoangamizwa ama kushtakiwa katika mahakama ya haki.

Msikiti huo ni muhimu sana kwa pande zote mbili kwa sababu Abu bakr al-Baghdad ndio alipotoa hutuba ya hadharani kama kiongozi wa IS siku chache tu baada ya kundi hilo la Jihad kutangaza uongozi wa Kiislamu takriban miaka mitatu iliopita.

Wapiganaji hao wa IS sasa wanatoroka nchini Iraq , nchi Jirani ya Syria ambapo wapiganaji wa kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani wanauzunguka mji wa Raqqa.

Msemaji wa muungano huo alituma ujumbe wa Twitter akisema kwamba eneo lenye ukubwa wa kilomita 84,000 mraba limekombolewa huku zaidi ya watu milioni nne wakiachiliwa huru kutoka kwa uongozi wa IS, akiongezea kuwa uongozi huo wa kidini unaangamia.