Wanamazingira waonya kuhusu mradi wa kawi Tanzania

Rais Magufuli amewataka wananchi wa Tanzania kuunga mkono mradi huo
Image caption Rais Magufuli amewataka wananchi wa Tanzania kuunga mkono mradi huo

Mradi tete wa kawi ya umeme unaotarajiwa kujengwa katika turathi za Tanzania unahatarisha wanyama pori na kipato cha mamia ya maelfu ya raia wanaotegemea eneo hilo, limeonya shirika la kimataifa la uhifadhi wa wanyama pori WWF.

Taifa hilo la Afrika mashariki linapanga kujenga mradi mkubwa wa kawi katika eneo la Stiegler Gorge katika turathi za UNESCO, iliopo katika eneo la uhifadhji wa wanyamapori la Selous kwa lengo la kuimarisha sekta yake ya kawi mbali na kumaliza uhaba wa kawi nchini humo.

Utafiti uliofanywa na WWF umeonya kwamba njia inayotumiwa na wanyama pori wakati wapohamia maeneo mengine itakatwa huku watu 200,000 wanaotegemea eneo hilo kwa kipato wakiathiriwa na mradi huo.

Bwana la umeme linatarajiwa kujengwa katika turathi hizo za UNESCO lenye ukubwa wa taifa la Switzerland ambalo ni maarufu kwa wanyama tofauti.

Wiki iliopita ,rais wa Tanzania John Pmbe Magufuli aliweka wazi kwamba hakuna pingamizi yoyote itaizuia serikali yake kujenga mradi huo.

''Naelewa kwamba mradi huu wa Stiegler Gorge utapingwa na wengi.

Utapingwa kwa sababu eti kuna maswala ya mazingira ambayo yanapaswa jkuangaziwa na wengine watasema kwa sababu unajengwa katika mbuga ya uhifadhi wa wanyama pori ya Selous.Mradi huu utakabiliwa na pingamizi chungu nzima lakini nawataka raia wa Tanzania kutahabiti ili kuhakikisha kuwa mradi huu unafanikiwa''.

Rais Magufuli amesema kwamba mradi huo ni muhimu kwa kawi ya taifa hilo wakati huu ambapo taifa hilo linapigania kuimarika kiviwanda.

Kufikia sasa taifa hilo lenye idadi ya watu milioni 53 lina Megawati 1400 ya umeme.

Bwawa hilo linakadiriwa kutoa Megawati 2000 za umeme.

Rais pia amesema kwamba mradi huo utachukua asilimia 3 pekee ya eneo hilo la uhifadhi wa wanyama pori ,akiwashutumu wakosoaji kwa kuongezea chumvi madhara ya mradi huo.

Shirika la kimataifa la uhifadhi wa wanyama pori WWF, limesema kuwa linaitaka serikali kufanya utafiti wa kina wa mazingira katika eneo hilo ili kuhakikisha madhara yote yanabainika kabla ya mipango yoyote ya mradi huo kuanza.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu dola bilioni mbili za Marekani.Haijulikani ni lini utaanza kutekelezwa.