Sudan Kusini yaomba walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania

Makamu wa kwanza wa rais nchini Sudan Kusini Taban Deng Gai. Haki miliki ya picha EPA
Image caption Makamu wa kwanza wa rais nchini Sudan Kusini Taban Deng Gai.

Serikali ya Sudan Kusini imeoimba Tanzania kuisaidia katika utoaji wa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wake hasa wa sekta ya afya, kilimo na kupatiwa walimu wa lugha la Kiswahili.

Makamu wa Kwanza Rais wa Serikali ya Sudan Kusini Jenerali Taban Deng Gai amesema taifa hilo linataka kuanza kufundisha lugha hiyo kwenye shule mbalimbali nchini humo.

Ametoa maombi hao baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kando mwa Mkutano 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa Ethiopia.

Jenerali Taban Deng ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Sudan Kusini kupitia Jumuiya mbalimbali hususan Jumuiya ya Afrika Mashariki katika juhudi zake za kutafuta amani ya kudumu pamoja na kuwavumilia kadri inavyowezekana hasa wanapopitia changamoto mbalimbali kufikia amani hiyo.

Kiongozi huyo amesema Tanzania ni mdau muhimu wa maendeleo kwa taifa hilo changa barani Afrika hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali ya Tanzania kuendelea kulisaidia taifa hiyo ili liweze kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na uimarishaji wa utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi wake.

Bi Suluhu Hassan amesema ili Tanzania iweze kushirikiana vizuri na Serikali ya Sudan Kusini ni muhimu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiriano wa Kimataifa za nchi hizo Mbili kuandaa mfumo maalum wa ushirikiano na utekelezaji wake.

Amesema mfumo huo utaainisha maeneo ya kushirikiana katika sekta mbalimbali kutokana na taifa hilo changa barani afrika kuwa na changamoto nyingi hasa kwenye sekta za afya, elimu, kilimo, siasa, ulinzi na usalama.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii