Uingereza: Saudia inafadhili watu wenye itikadi kali nchini Uingereza

Msikiti Saudia Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Uingereza yasema Saudia inafadhili makundi yenye itikadi kali

Saudia ndio mfadhili mkuu wa watu wenye misimamo mikali ya kidini nchini Uingereza kulingana na ripoti mpya.

Ripoti hiyo ya Henry Jackson Society imesema kuwa kuna ushirikiano wa wazi kati ya mashirika ya Kiislamu yanayotoa ufadhili kwa wahubiri wenye chuki na makundi ya kijihad yanayokuza ghasia.

Idara ya maswala ya kigeni ilitaka kuchunguzwa kwa jukumu la Saudia na mataifa mengine ya Ghuba.

Ubalozi wa Saudia nchini Uingereza unasema kuwa madai hayo ni ya ''uongo''.

Mawaziri wanakabiliwa na shinikizo ya kuchapisha ripoti ya makundi ya Kiislamu yalioko nchini Uingereza.

Ripoti hiyo ya Idara ya maswala ya ndani kuhusu uwepo wa makundi ya kijihad ilioanzishwa na aliyekuwa waziri mkuu David Cameron 2015 bado haijakamilika huku kukiwa na ripoti za iwapo itachapishwa.

Wakosoaji wanasema kuwa huenda ikawa vigumu kwa serikali kuisoma, kutokana na ushirikiano wa karibu wa kidiplomasia, usalama, kiuchumi na mataifa ya Ghuba hususan Saudia.

Ripoti hiyo ya siku ya Jumatano inasema kuwa mataifa kadhaa ya Ghuba ikiwemo Iran yanatoa ufadhili wa kifedha kwa misikiti na taasisi za elimu ya Kiislamu ambazo zimekuwa zikiwakuza wahubiri wa chuki swala linalosababisha kuenea kwa Itikadi kali.

Katika kilele cha orodha hiyo , ripoti hiyo inasema ni Saudia.

Inadai kwamba watu binafsi na wakfu wamehusishwa kueneza itikadi za Wahabby ikinukuu mifano kadhaa.

Katika visa vyengine vichache, ripoti hiyo inadai taasisi nchini Uingereza zinazopokea ufadhili wa Uingereza zinatekeleza operesheni zake moja kwa moja kutoka Saudia ,ijapokuwa fedha hizo huonekana kununua ushawishi wa wafadhili wa kigeni.

Katika taarifa ,ubalozi wa Saudia mjini London unasema kuwa tuhuma zozote kwamba ufalme huo unafadhili watu wenye itikadi kali hazina msingi na hazina ushahidi wowote.

Imesema kuwa taifa hilo limeshambuliwa na al-Qaeda na wapiganaji wa Islamic State.

Imeongezea: Hatuungi mkono na hatuwezi kuunga mkono vitendo vya makundi yenye itikadi kali na hatutapumzika hadi makundi hayo yaliokosa mwelekeo na mashirika yao yaangamnizwe.