Mwandishi atoweka kabla ya kuzindua kitabu chake Kenya

Mwandishi atoweka kabla ya kuzindua kitabu chake Kenya
Image caption Mwandishi atoweka kabla ya kuzindua kitabu chake Kenya

Mwandishi wa kitabu cha "The Raila Conspiracy" kinachosimulia jinsi tawala za viongozi tofauti wa Kenya wamekuwa wakiiba kura kupitia kwa njama fiche, ya kumnyima madaraka kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga ametoweka.

Jamaa na marafiki wake wanasema kuwa Newton Babior hajaonekana tangu Juni 27 siku aliyotarajiwa kuzindua kitabu hicho.

Wageni waheshimiwa katika uzinduzi huo walikuwa ni Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA Raila Odinga, ambaye ndiye mhusika mkuu katika chapisho hilo lililosisimua wachaganuzi wa siasa.

Babior alikuwa ameahidi kufika kwa uzinduzi huo siku aliyotarajiwa lakini akatoweka huku simu yake ikizimwa. Serikali kupitia kwa msemaji wa polisi imesema kuwa haina habari zozote kumhusu mwandishi huyo ila juhudi zinafanywa ilikubaini alipo.

"Mtu yeyote anayetoweka kwa hali yeyote ile ,inatuhusu kama polisi. Kama huyu bwana ametoweka pasi na mapenzi yake na jamaa wake wamepiga ripoti kwa polisi bila shaka tutalishughulikia ipasavyo kumtafuta awe hai au ameaga dunia. Hata hivyo tunaomba kuwa tutampata angali hai" alisema msemaji wa polisi Charles Owino.

Katika kitabu hicho chake Newton Babior alikuwa anaelezea kinaga ubaga kuhusiana na njama ya kumnyima uongozi kiongozi wa upinzani kwa misingi ya kuiba kura.

Babior anadai kuwa uchaguzi wa mwaka wa 2002 ulioshuhudia uchaguzi wa Mwai Kibaki kuwa rais wa Kenya ndio wa pekee uliokuwa huru.

Kitabu hicho kinaongezea kuwa chaguzi za mwaka wa 2007 na 2012 ziliibwa ili kumnyima madaraka kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Hata hivyo duru zinazotofautiana na habari hii zinasema kuwa mwandishi huyo huenda alikosa uwepo wa mhusika mkuu wa kitabu hicho Raila Odinga na hivyo akaibua mbinu ya kukinadi kwa kudanganya kuwa ametoweka. Na kuhusiana na hilo msemaji wa polisi amesema uchunguzi utafanywa