Kenyatta na Odinga wajiondoa katika mdahalo wa wagombea Kenya

Wagombea wote walishiriki mdahalo wakati wa uchaguzi wa 2013 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wagombea wote walishiriki mdahalo wakati wa uchaguzi wa 2013

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamejiondoa kutoka kwenye mdahalo wa moja kwenye runinga wa wagombea urais nchini humo.

Mdahalo huo ulikuwa umepangiwa kufanyika Julai 10 na marudio Julai 24.

Lakini wagombea hao wamesema hawatahudhuria mdahalo huo kwa sababu hawakushirikishwa wakati wa maandalizi ya mdahalo huo.

Rais Kenyatta, wa chama cha Jubilee, alikuwa wa kwanza kutangaza kujiondoa.

Katibu mkuu wa chama hicho Raphael Tuju alisema waandalizi wa mdahalo huo hawakuwasiliana rasmi na maafisa wa ikulu au chama cha Jubilee rasmi kuhusu mdahalo huo.

Bw Tuju alisema mdahalo huo unaadaliwa "kupitia matangazo kwenye vyombo vya habari na watu ambao hatuwafahamu."

Saa chache baada ya hatua ya chama hicho tawala, muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA) ulitangaza kuwa Bw Odinga pia hatahudhuria.

"Mgombea urais wa NASA Raila Odinga hatashiriki katika mdahalo wa urais wa 2017 chini ya mpangilio wa sasa uliopendekezwa," taarifa kutoka afisa wa mawasiliano wa Bw Odinga Salim Lone ilisema.

"Hata hivyo, Baraza la Kampeni la mgombea urais wa NASA linamhimiza Rais Uhuru Kenyatta awe tayari kushiriki mdahalo na Raila Odinga kuhusu masuala yanayoathiri Wakenya kwa sasa."

Mdahalo huo umekuwa ukiandaliwa na kampuni kwa jina Debates Media Limited.

Mgombea urais mwingine Abduba Dida tayari ameishtaki kampuni hiyo pamoja na Baraza la Taifa la Vyombo vya Habari.

Bw Dida anataka wagombea wote washiriki mjadala kwa pamoja badala ya kutenganishwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii