Watuhumiwa elfu nne wa mihadarati wamekamatwa Tanzania

Bw Majaliwa Haki miliki ya picha Getty Images

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema maafisa wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) wamewakamata watuhumiwa 4,809 wa mihadarati katika kipindi cha miezi minne.

Waziri Mkuu amesema hayo mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11 hadi Septemba 5, mwaka huu.

"Katika kipindi kifupi tangu Februari, 2017 Mamlaka hii ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroini (gramu 327.173); kokeni (kilo 26.977); bangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo 11,306.67) na lita 6,338 za kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini," amesema.

Amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bangi na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi na kazi hiyo inaendelea.

Kutokana na hatua hizo, jumla ya majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.

"Dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya."

Tanzania imekuwa ikizidisha juhudi za kukabiliana na matumzii ya dawa za kulevya nchini humo.

Wiki chache zilizopita, watu mashuhuri walikamatwa na kuhojiwa na polisi wakituhumiwa kuhusika katika ulanguzi wa dawa hizo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii