Trump aonya Korea Kaskazini anafikiria kuchukua 'hatua kali'

Donald Trump Warsaw Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Trump amesema Korea Kaskazini wana tabia mbaya sana

Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Korea Kaskazini kwamba anapanga kuchukua hatua kali dhidi ya jaribio la kombora la masafa marefu .

''Wana tabia hatari sana, hatari sana na lazima jambo lifanywe kuhusu hili," alisema.

Lakini baadaye kidogo alitoa matamshi ya msimamo wa kadri akisema: Tutaangalia kile kitakachofanyika katika kipindi cha wiki na miezi ijayo.

Pyongyang ilifanyia majaribio kombora la masafa marefu lililo na uwezo wa kufika katika jimbo la Alaska nchini Marekani siku ya Jumapili.

Licha ya kombora hilo kuruka kwa dakika chache na kuanguka baharini, jaribio hilo limetajwa kuwa uchokozi mbaya na Marekani.

''Nina orodha ya hatua kali tunazofikiria kutumia'', Bw Trump alisema kuhusu hatua itakayochukuliwa na Marekani. "Lakini hii haina maana kwamba ni lazima tuchukue hatua hizo

Alisema kuwa mataifa mengine pia yanafaa kuipa changamoto Korea Kaskazini kutokana na tabia yake mbaya.

Bwana Trump alikuwa akizungumza mjini Warsaw nchini Poland katika mkutano wa pamoja na rais wa Poland Adrsej Duda.

Anatarajiwa kukutana na viongozi wengine katika mkutano wa mataifa yenye uwezo mkubwa duniani G20 nchini Ujerumani siku ya Ijumaa.

Matamshi hayo ya rais yanajiri baada ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley kuliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Marekani iko tayari kutumia uwezo wake wa kijeshi dhidi ya Korea kaskazini ''iwapo itahitajika'' kufanya hivyo.

Marekani na Korea Kusini tayari zimezidisha mazoezi ya kijeshi ya pamoja, wakirusha makombora katika bahari ya Japan katika kile kinaoonekana kuwa onyesho la uwezo wake.

Pyongyang ha tahivyo imesema kuwa haitafanya majadiliano kuhusu mpango wake wa makombora hadi pale Marekani itakapositisha sera yake ya uadui dhidi ya Korea Kaskazini.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Meli ya kivita ya Korea Kusini Yang Manchun ilionekana ikirusha makombora ya kushambulia meli

Jaribio hilo la kombora la masafa marefu linaloweza kuruka hadi bara nyingine lilikuwa ni ukiukaji tena wa marufuku ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Lakini China na Urusi zina kura batili na zinapinga kuchukuliwa kwa hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini.

Rais Trump tayari ameikosoa China kwa kuendelea kufanya baishara na Pyongyang.

Kiongozi huyo wa Marekani anapangiwa kukutana na Rais wa China Xi Jinping katika mkutano wa viongozi wa nchi za G20 wiki hii.

Jamii ya kimataifa imeungana kuhusu hili?

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in ameeleza wasiwasi wake kuhusu mpango wa makombora na silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini na kusema kwamba taifa hilo linapiga hatua haraka sana kuliko ilivyotarajiwa.

Akiongea Berlin Jumatano, ambapo alikutana na kiongozi wa Ujerumani Angela Merkel, alisema watatafakari uwezekano wa kuongezea taifa hilo vikwazo.

Katika mkutano wa Baraza la Usalama la UN mjini New York, balozi wa Ufaransa alisema taifa lake pia linaunga mkono wazo la kukaza vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.

Urusi, ambayo ilishutumu jaribio hilo la kombora, ilisema hakufai kufikiriwa hatua ya kijeshi.

Balozi wa Uchina Liu Jieyi alikariri msimamo huo wa Urusi.

Korea Kaskazini inasemaje?

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA lilisema "mkakati wa Marekani wa kutumia ubabe" pamoja na shinikizo na kushirikisha wengine "hautafanikiwa".

Taarifa hiyo ilsiema ni lazima Marekani ikomeshe sera yake ya uchokozi na uadui ndipo Korea Kaskazini ikubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un alikuwa awali amenukuliwa akisema kwamba jaribio la Jumanne lilikuwa "zawadi" kwa Wamarekani Siku yao ya Uhuru, na kwamba aliwaagiza maafisa wake kuwa "wakituma vifurushi vidogo na vikubwa vya zawadi mara kwa mara" kwa Wamarekani.

Pyongyang ilisema kombora lake la Hwasong-14 ICBM ililolifanyia majaribio lilifikia upeo wa 2,802km (maili 1,731) juu angani na lilipaa umbali wa 933km kwa dakika 39 kabla ya kushambulia shabaha baharini.

Korea Kaskazini imesema sasa "ni taifa kamili lenye nguvu za silaha za nyuklia na ina roketi yenye nguvu zaidi ya kurusha makombora kutoka bara moja hadi nyingine duniani na kwamba makombora yake yanaweza kushambulia eneo lolote duniani.

Lakini ingawa wataalamu wanaafikiana kwamba jaribio hilo la kombora linaonesha Pyongyang ina kombora la masafa marefu, wanatilia shaka uwezo wa makombora hayo kubeba vichwa au mabomu ya nyuklia.


Kombora la ICBM hufanya kazi vipi?

  • Ni kombora la masafa marefu lililoundwa kubeba kichwa au bomu la nyuklia
  • Linaweza kupaa zaidi ya 5,500km (maili 3,400), ingawa makombora mengi hupaa zaidi ya 10,000km
  • Pyongyang awali imeonesha aina mbili za makombora ya ICBM: KN-08, lenye uwezo wa kusafiri 11,500km, na KN-14, lenye uwezo wa kusafiri 10,000km, lakini kabla ya 4 Julai haikuwa imesema wkamba imefanyia majaribio kombora la ICBM. Haiko wazi ni nini tofauti kwenye Hwasong-14.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii