Donald Trump na Vladmir Putin kukutana ana kwa ana G20

Donald Trump na Vladmir Putin kukutana ana kwa ana G20
Image caption Donald Trump na Vladmir Putin kukutana ana kwa ana G20

Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin wanatarajiwa kukutana ana kwa ana katika mkutano wa mataifa yalio na uwezo mkubwa duniani G20 katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani.

Wawili hao wamesema kwamba wanataka kuimarisha uhusiano wao ambao uliharibika katika mgogoro wa Syria na Ukraine mbali na madai ya Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani.

Kabla ya mkutano huo maafisa wa polisi 76 walijeruhiwa katika makabiliana na waandamamanaji .

Mikutano mikubwa ya hadhara inatarajiwa siku ya Ijumaa.

Viongozi wakuu duniani pia wanakabiliwa na misimamo tofauti kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Je ni maswala gani yatakayozungumziwa katika mkutano wa Trump-Putin?

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana Ijumaa mchana kandakando ya mkutano wa G20.

Vyombo vya habari nchini Urusi vimesema kuwa mkutano huo utakuwa kwa saa moja , lakini baadaye ripoti zinasema kuwa huenda ukachukua dakika 30.

Marais hao wanatarajiwa kujadiliana sana kuhusu maswala ya Syria na Ukraine.

Siku ya Alhamisi ,bwana Trump alitumia hotuba yake nchini Poland kutoa wito kwa Urusi kuwacha kuyumbisha Ukraine na mataifa mengine.

''Moscow pia ni lazima isitishe usaidizi kwa serikali mbaya kama vile Syria na Iran na kujiunga na jamii ya mataifa yanayowajibika'', alisemaTrump.