Bintiye Trump aketi katika kiti cha babake G20

Ivanka Trump alimwakilisha babake kwa muda Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Ivanka Trump alimwakilisha babake kwa muda

Katika hatua isiyo ya kawaida, binti yake Bwana Trump, Ivanka, alikaa kwa niaba ya baba yake wakati wa kikao kinachohusu Afrika kwenye mkutano wa nchi tajiri wa G20.

Vikao vya asubuhi vililenga masuala muhimu ya uhamiaji na afya.

Picha iliyowekwa twitter na mmoja wa wapatanishi kutoka Urusi ilimwonyesha Ivanka Trump akikaa katikati ya Rais wa China Xi Jinping na waziri mkuu wa Uingereza, Bi Teresa May.

Mwandishi wa BBC katika mkutano huo anasema hakumbuki kuwepo na mipango kama hiyo hapo zamani na kiongozi wa nyadhifa ya juu kama vile waziri wa mambo ya nje, ndio aghlabu huchukua nafasi ya Rais.

Bi Trump hakuonekana akishiriki katika mchango wowote kuhusu uhamiaji wa raia wa Afrika kuelekea Ulaya na afya wakati babake alipokuwa ameondoka.

Picha ya uwepo wake ilichapishwa katika mtandao wa Twitter na mshiriki mmoja wa Urusi na kuzua hisia kali katia mitandao ya kijamii.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo walisema kuwa bi Trump hajachaguliwa wala kukaguliwa sifa zake kama mmiliki wa kampuni ya fesheni kustahili kukaa katika kikao kama hicho chenye hadhi ya juu ya kidiplomasia.

Wengine walimkosoa hadharani kwa kuwa miongoni mwa viongozi wakuu baada ya madai yake katika mahojaino kwamba hujaribu kutojishirikisha katika siasa.

Bi Trump alikuwa amejiunga na babake kwa mkutano wa awali wa G20 siku ya Jumamosi kuhusu wanawake, biashara na fedha pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Christine Lagarde, mkurugenzi wa hazina ya fedha duniani IMF.

Wanawake wote watatu hapo awali walikuwa pamoja wakati wa kikao cha G20 kuhusu wanawake mjini Berlin mwezi April.

Binti wa Trump akana kuwa na nafasi nyeti ikulu

Wakati huo alimtetea babake kama mtu ambaye anapenda kuzaidia familia kuendelea.

Bwana Trump alirudi baadaye ili kuchukua kiti chake kilichokuwa kati ya waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na rais wa China Xi Jinping.