Trump: Putin alikana kuingilia uchaguzi wa Marekani

Vladimir Putin and Donald Trump Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bwana Putin (kushoto) na Bwana Trump walikutana Ijumaa nchini Ujerumani

Rais wa Marekani Donald Trump anasema kuwa ni wakati wa kushirikiana na Urusi baada ya mkutano wake na rais wa Urusi Vkladimir Putin.

Aliandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa Putin alikana kabisa kuvuruga uchaguzi wa Marekani wakati walikutana uso kwa uso kwenye mkutano wa G20 siku ya Ijumaa.

Lakini msimamo huo wa Trump unaenda kinyume na ule wa baadhi ya maafisa wake wa vyeo vya juu.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley, anasema kuwa Marekani kamwe haiwezi kuiamini Urusi.

Naye waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Mareknai Rex Tillerson, alisema kuwa hatua ya Urusi kuvuruga uchaguzi wa mwaka 2016 imesalia kikwazo kikubwa kwenye uhusiano wake na Urusi.

Mwendesha mashtaka maalum anachunguza ikiwa washirika wa Trump walishirikiana na jitihada za Urusi kushawishi uchaguzi wa Marekani wa Mwezi Novemba.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, alisema kuwa Bwana Trump alikubali jibu la Putin kuwa madai hayo si ya ukweli

Mada zinazohusiana