Gati la watumwa la Valongo nchini Brazil latambuliwa na Unesco

Valongo, Rio de Janeiro, Brazil, Juni 28, 2017. Haki miliki ya picha AFP
Image caption Eneo hilo lilikuwa limefunikwa kwa uwanja, barabara na maegesho ya magari

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, sayansi na utamaduni limetambua gati la Rio de Janeiro ambalo lilitumiwa kupakua zaidi ya watumwa milioni moja kutoka Afrika kuwa turathi ya ulimwengu.

Gati hilo la Valongo lilitumiwa kwa karne tatu na lilikuwa kiingilio kikuu zaidi cha watumwa kutoka Afrika kuingia Brazil.

Mabaki ya gati hilo yaligunduliwa wakati wa shughuli za ujenzi kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya 2016.

Watumwa wengi kutoka Afrika walipelekwa Brazil.

Baada ya safari ndefu kupitia bahari ya Atlantiki, watumwa kutoka Afrika waliokuwa wamedhoofika waliwekwa kwenye gati hilo wapate nafuu na kuongeza uzani kabla ya kuuzwa katika masoko ya watumwa.

Wengi walifariki na kuzikwa katika makaburi yaliyo karibu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Claudio Honorato ni mhifadhi wa mambo ya kale eneo la makaburi ya Valongo

Unesco imesema gati la Valongo linafaa kuwa na hadhi sawa na Hiroshima na Auschwitz katika historia "kutuwezesha kukumbuka sehemu ya historia ya binadamu ambayo haifai kusahauliwa."

Wengi wa raia wa Brazil hawakufahamu umuhimu wa eneo hilo hadi miaka michache iliyopita.

Mabaki ya gati hilo yaligunduliwa kibahati mwaka 2011, familia moja iliyokuwa ikikarabati nyumba ilipogundua kaburi la halaiki lililojaa mifupa na mafuvu ya binadamu.

Gati hilo lilijengwa mwaka 1779 kuhamisha biashara ya utumwa kutoka katikati mwa mji.

Image caption Wengi wa watumwa wa zamani walijenga makao eneo hilo ambalo sasa hufahamika kama Afrika Ndogo

Kati ya 1770 na 1830, maelfu ya watumwa walizikwa makaburi yaliyo karibu na gati hilo.

Biashara ya utumwa ilipigwa marufuku 1831 baada ya Brazil kujitangazia uhuru kutoka kwa Ureno.

Lakini biashara iliendelea kwa njia haramu hadi 1888.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii