Odinga yuko buheri wa afya sasa, mshauri wake asema

Bw Odinga amesema iwapo atashinda, serikali yake itakuwa ya mpito
Image caption Bw Odinga

Mgombea urais wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amepata nafuu kabisa baada ya kulazwa kwa muda jana, mshauri wake mkuu amesema.

Bw Odinga alilazwa hospitalini Mombasa Jumapili jioni baada ya kuhisi maumivu tumboni.

Alichunguzwa na madaktari lakini akaruhusiwa kuondoka muda mfupi baadaye.

Mshauri wake Bw Salim Lone amesema Bw Odinga yuko buheri wa afya na alikuwa mchangamfu ndege iliyombeba kutoka Mombasa ilipotua katika uwanja wa Wilson, Nairobi usiku wa manane.

"Nilizungumza na Bw Odinga tena asubuhi hii na alikuwa mchangamfu. Alipigia simu watu kadha, akiwemo mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) Wafula Chebukati," amesema Bw Lone.

Kwa mujibu wa afisa huyo, kiongozi huyo wa upinzani alianza kuhisi matatizo tumboni adhuhuri akiwa Kilifi na alipokuwa anatua uwanja wa ndege wa Mombasa maumivu yalikuwa yamezidi.

Madaktari Mombasa walimpima na kumuongezea maji mwilini.

Amesema Bw Odinga anashuku matatizo yake yalitokana na samaki aliyemla mchana.

"Wenzake hawakula chakula hicho," amesema.

Hii si mara ya kwanza kwa Bw Odinga kulazwa kutokana na chakula chenye sumu.

Mwezi Machi, alikimbizwa hospitalini Karen na kutibiwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii