Kikao cha tume ya uchaguzi na wagombea chatibuka Kenya

Wafula Chebukati
Maelezo ya picha,

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya Wafula Chebukati

Kikao cha Tume ya uchaguzi nchini Kenya cha kupokea maoni ya umma juu ya suala tata la utoaji wa zabuni ya utengenezaji wa karatasi za uchaguzi mkuu kimetibuka.

Wagombea urais na wawakilishi wa wagombea urais hawakusikilizana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati kuhusu zabuni tata ya uchapishaji wa karatasi za kura iliyosimamishwa na mahakama wiki jana.

Mkutano huo ulionekana kukosa mwelekeo wengi wa waliohudhuria wakihoji mbona wagombea urais waliitwa kujadili suala ambalo tume ya uchaguzi tayari imekata rufaa mahakamani baada ya kupoteza kesi mahakamani.

Kujadili zabuni hiyo ni kinyume cha sheria, walisema.

Mgombea huru wa Urais Ekuru Aukot alitoka katikati ya mkutano akisema kwamba hana muda wa kupoteza kwenye kikao ambacho hakina mbele wa nyuma, wakati huo anaenda kutumia kutafuta kura kwa kufanya kampeni.

Rais Uhuru Kenyatta Jumapili alionekana kukemea mahakama kwa kuweka vizuizi tunapoelekea kufanya uchaguzi huku akisema kwamba hatokubali uchaguzi kuahirishwa.