Waziri wa zamani Tanzania arejesha mamilioni kuhusiana na kashfa ya Escrow

William Ngeleja
Image caption Mbunge wa Sengerema aliwaonesha wanahabari risiti ya malipo ya fedha jijini Dar es Salaam

Sakata ya akaunti ya Escrow imechukua mwelekeo mpya nchini Tanzania baada ya mmoja wa walionufaika na mgao wa fedha zinazohusishwa na kashfa hiyo kujitokeza na kutangaza kuzirudisha fedha hizo kwa serikali.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu, William Ngeleja, ambaye ni mbunge wa Sengerema, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, alisema ameamua kuzirudisha fedha hizo baada ya kugundua kwamba aliyempatia fedha hizo anahusika na kashfa ya akaunti ya Escrow.

"Kwa vile sasa imedhihirika kwamba aliyenipa msaada huu anatuhumiwa kwenye kashfa ya akaunti ya Escrow, nimepima na kutafakari, na hatimaye nimeamua, kwa hiari yangu mwenyewe, kurejesha serikalini (Kwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania, TRA) fedha zote nilizopewa kama msaada bila kujali kwamba nilishazilipia kodi ya mapato", inasema sehemu ya taarifa aliyoitoa Bw Ngeleja

Mbunge huyo, ambaye aliwahi kuwa waziri wa nishati nchini Tanzania, pia aliwaonyesha waandishi wa habari nakala ya risiti ya malipo ya fedha kiasi cha TSH 40.4 milioni, sawa na takribani Dola 20,000 ikiwa ni malipo aliyoyafanya kwa mamlaka ya mapato Tanzania

Hatua hii ya kurudisha fedha inakuja siku chache baada ya watuhumiwa wawili wa kashfa hiyo kufikishwa mahakami kwa makosa ya kuhujumu uchumi

Maswali mengi yanaendelea kuibuka kuhusiana na hatua ya Ngeleja kurudisha fedha hizo lakini vyombo vya habari nchini Tanzania vinaripoti kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini humo imesema ni mapema kuzungumzia suala la uwezekano wa kusamehewa kwa vigogo watakaorudisha fedha zinazohusishwa na sakata hiyo ya Escrow

Mada zinazohusiana