Barua pepe yaibuka kumhusisha Trump Junior na Urusi

Donald Trump Jr at Trump Tower in New York City, 18 January 2017 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Trump Jr anasisitiza kuwa wakili huyo hakutoa taarifa muhimu kumhusu Bi Clinton

Mtoto wa kiume wa rais wa Marekani Donald Trump, Donald Trump Jr , aliambiwa kuwa taarifa kumhusu Hillary Clinton ambayo angepewa na wakili wa Urusi, ilikuwa sehemu ya jitihada za Urusi kumsaidia babake katika kampeni ya uchaguzi

Rob Goldstone ambaye alipanga mkutano huo wa Juni mwaka 2016, aliandika hayo kupitia barua pepe.

Bwana Trump Jr alitetea hatua ya kuhudhuria mkutano huo akisema kuwa ahadi ya taarafa potovu aliyopewa haikuwepo.

Trump Jr amekana kutoa habari za kukanganya kuhusu mkutano huo wa mwaka uliopita.

Pia amesema kuwa lilikuwa jambo la kawaida kupata taarifa kuhusu wagombea pinzani.

Maafisa nchini Marekani wanachunguza madai yanayohusu Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani.

Mkwe wa Trump Jared Kushner na aliyekuwa mkuu wa kampeni Paul J Manafort, walikuwa pia katika mkutano huo na Natalia Veselnitskaya.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jared Kushner hajazungumza kuhusu taarifa ya Donald Trump Jr

Trump Jr anasisitiza kuwa wakili huyo hakutoa taarifa muhimu kumhusu Bi Clinton, ambaye alikuwa mshindani wa babake katika kiti cha urais.

Mkutano huo ulifanyika tarehe 9 mwezi Juni mwaka 2016 katika jengo la Trump Tower, wiki mbili baada ya Donald Trump kupata uteuzi wa Republican.

Unaaminiwa kuwa mkutano wa kwanza wa siri kati ya raia wa Urusi na watu waliokuwa karibu na Bwana Trump.

Baada ya New York Times kuripoti mara ya kwanza kuhusu mkutano huo siku ya Jumamosi, Bwana Trump Jr alitoa taarifa iliyothibitisha kuwa mkutano huo ulifanyika lakini haikutaja ikiwa ulihusu kampeni ya kuwania urais

Mada zinazohusiana