Walimu wakuu wakamatwa kwa kukutana na al-Shabab Somalia

Wapiganaji wa al_Shabab
Image caption Wapiganaji wa al_Shabab

Walimu wakuu kutoka shule saba za kibinafsi nchini Somalia wamekamatwa kwa kukutana na wapiganaji wa al-Shabab ili kujadiliana kuhusu mabadiliko kadhaa katika mtaala wa shule hizo ,waziri wa maswala ya ndani ameambia BBC.

Al Shabab walitoa taarifa mnamo mwezi Aprili na kutishia kuwaadhibu walimu na wazazi ambao wanawapatia wanafunzi elimu ya kidunia.

Walimu hao saba kutoka mji wa Jowhar watashtakiwa kwa kukutana na wanachama wa kundi haramu , waziri wa elimu kutoka jimbo la Hirshabelle ,Mahad Hassan Osman aliambia BBC Somalia.

Aliongezea kuwa shule zilitarajia kufuata mitaala ya elimu ya kawaida na haziwezi kubadilisha kufuatia shinikizo ya kundi la Alshabab.

Bwana Osman alisema kuwa walimu hao walikamatwa kilimota 15 nje ya Jowhar walipokuwa wakirudi kutoka kwa mazungumzo hayo na wapiganaji hao.

Walifanya mikutano na wapiganaji hao na kujaribu kubadilisha mtaala wa shule ili kuafikia kile kundi hilo linachotaka ambacho ni kuidhinishwa kwa sheria kali za Kiislamu.Eneo linalodhibitiwa na wapiganaji hao nje ya Jowhar ,ambalo liko kilomita 90 kutoka mji mkuu wa Mogadishu.