Rwanda yashutumiwa kwa kuwaua 37 wenye makosa madogo

Baadhi ya watu waliodaiwa kuuawa kwa kufanya makosa madogo Haki miliki ya picha Human Rights Watch
Image caption Baadhi ya watu waliodaiwa kuuawa kwa kufanya makosa madogo

Vikosi vya usalama nchini Rwanda vimewaua takriban watu 37 wanaoshukiwa kufanya makosa madogo madogo tangu mwezi Aprili 2016 kulingana na ripoti ya Human Rights Watch HRW.

Ripoti hiyo inasema kuwa hatua hiyo inaonekana kuwa mpango wa makusudi kuwaua washukiwa wa wizi.

Mashahidi wameambia HRW kwamba hatma ya mtu mmoja anayetuhumiwa kuiba ng'ombe iliamuliwa katika mkutano wa kijamii.

Fulgence Rukundo alihojiwa kuhusu ng'ombe alioiba na baadaye kuchukuliwa katika mkutano wa meya wa wilaya.

Mtu mmoja alielezea kile kilichotokea:

Wakati mkutano huo ulipokamilika, wanajeshi walimpeleka Fulgence katika uwanja mdogo karibu na mgomba .Tulikuwa wengi ambao tulikuwa tukifuata nyuma wengine wakiwa wanafunzi wa shule ya msingi.Tulitaka kuona kile kitakachotokea.Mwanajeshi mmoja alimwambia kusimama na kutembea, na wanajeshi wengine wakatuambia tuondoke.Wakati huo nilisikia milio mitatu ya risasi.

Mashahidi wengine waliambia HRW kwamba wengine waliouawa walituhumiwa kw kuiba ndizi, pikipiki, kuingiza bangi kupitia mpaka wa taifa hilo na DR Congo ama hata kutumia neti haramu za uvuvi.

Maafisa wa Rwanda walikana kwa HRW kwamba mauaji ya kiholela yalifanyika.

HRW ilisema mwaka 2015 kwamba pia ilikuwa imenakili kukamatwa maelfu ya watu wakiwemo watoto wa kurandaranda mitaani pamoja na makahaba.