China yaionya Botswana kuhusu Dalai Lama

Dalai Lama Haki miliki ya picha AFP

China imeitahadharisha Botswana dhidi ya kumkubalia kiongozi wa kidini wa Tibet anayeishi uhamishoni Dalai Lama kuzuru taifa hilo mwezi ujao, shirika la habari la Reuters linasema.

Dalai Lama anatarajiwa kuhutubia kongamano kuhusu haki za kibinadamu katika mji mkuu wa taifa hilo la kusini mwa Afrika, Gaborone, mwezi Agosti na pia amepangiwa kukutana na Rais Ian Khama.

Bw Geng Shuang, msemaji wa idara ya mambo ya nje ya China anaripotiwa kuambia kikao cha wanahabari jijini Beijing mapema leo kwamba Dalai Lama alitumia cheo chake kujihusisha katika shughuli ambazo ni za kuihujumu China.

"Tunatumai kwamba taifa hilo linaweza kutambua hasa Dalai Lama ni nani, na kuheshimu wasiwasi wa China, na hivyo kuchukua uamuzi mwafaka kuhusu suala hili," taarifa yake ilisema.

Dalai Lama aliikimbia Tibet na kutorokea India karibu miaka 60 iliyopita baada ya kufeli kwa maasi aliyoyaongoza dhidi ya utawala wa China.

Kwa muda mrefu, amekuwa na uadui na China.

Serikali ya China humuita mtu hatari anayetetea kujitenga kwa Tibet, shirika la habari la Reuters linasema.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii