Msafara wa rais Mugabe wahusika katika ajali ya barabarani

Rais Mugabe akiwa katika gari lake
Image caption Rais Mugabe akiwa katika gari lake

Mke wa rais wa Zimbabwe Grace Mugabe alipata majeraha madogo katika ajali ya barabarani, lakini rais Mugabe hakuumia popote.

Vyombo vya habari vya serikali vinasema ajali hiyo ilitokea wakati familia hiyo ilipokuwa ikitoka uwanja wa ndege wa Harare.

Walikuwa wamerudi kutoka Singapore ,ambapo rais huyo ameenda kufanyiwa ukaguzi wa matibabu.

Kulingana na mwandishi wa BBC nchini humo Shingai Nyoka mke wa rais Grace Mugabe alipata jeraha katika mkono wake katika kile serikali inasema ni ajali ndogo ya barabarani iliohusisha msafara wa rais.

Bi Mugabe alitibiwa katika kliniki moja na kuruhusiwa kwenda nyumbani bila majeraha makubwa.

Msemaji wa rais aliambia chombo cha habari cha serikali kwamba mke wa rais alilalamikia uchungu katika mkono wake lakini hakuelezea kiini cha ajali hiyo.

Shahidi mmoja anasema kuwa aliona mwili uliotengwa wa mwendeshaji pikipiki wa msafara wa rais katika eneo hilo.

Kumekuwa na makumi ya ajali yanayohusisha msafara huo wa rais katika kipindi cha miaka mitano iliopita.

Msafara huo una magari 10 yenye ving'ora vya kuyaonya magari mengine.