Msichana wa Ujerumani ''aliyejiunga na IS akamatwa Iraq''

Mji wa Mosul nchini Iraq Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mji wa Mosul nchini Iraq

Viongozi wa mashtaka nchini Ujerumani wanachunguza iwapo msichana wa miaka 16 kutoka Ujerumani ni miongoni mwa kundi la washukiwa wa Islamic State waliokamatwa mjini Mosul.

Aliripotiwa kupatikana na vikosi vya kijeshi katika handaki katika mji huo wa Iraq siku ya Alhamisi pamoja na raia wengine 19 wa kigeni.

Maafisa wanajaribu kuthibitisha iwapo ni msichana huyohuyo aliyepotea kutoka mji wa Ujerumani wa Lulsnitz mwaka uliopita.

Serikai ya Iraq imetangaza ushindi dhidi ya IS mjini Mosul ,ijapokuwa vita vinaendelea katika maeneo mengine ya mji huo wa zamani.

Vita hivyo ambavyo vimechukua miaka tisa viliyawacha maeneo makubwa yakiwa yameharibiwa na kuwaua maelefu ya raia huku takriban watu 920,000 wakiwachwa bila makao.

Picha za msichana huyo aliyekamatwa na wanajeshi wa Iraq zilichapishwa na vyombo vya habari vya eneo hilo.

Chombo cha habari cha Ujerumani DPA kiliripoti kuwa kundi hilo la wageni lilikuwa likimiliki silaha na mikanda ya vilipuzi wakati walipokamatwa.

Washukiwa hao wanashirikisha raia watano wa ujerumani , watatu wa Urusi , watatu wa Uturuki na wawili wa Canada.