Uchaguzi Kenya 2017: Darubini kupitia vijana watatu

Vijana

Takwimu za Tume ya Uchaguzi Kenya zinaonesha idadi kubwa ya wapiga kura nchini humo ni vijana. Tumewapata vijana watatu ambao mwaka huu itakuwa mara yao ya kwanza kupiga kura.

Wanafikiria nini kuhusu yanayojiri kwenye kampeni?

Watakuwa wakisimulia kila siku kuhusu yanayojiri na msimamo wao kuhusu masuala hayo.

1. Beatrice Waithera, 23, anaunga mkono muungano wa wagombea wadogo wa Thirdway Alliance.

Maelezo ya video,

Beatrice atamchagua rais mara ya kwanza Kenya

2. Martin Maina, 21, ni mwanafunzi jijini Nairobi na anaunga mkono chama tawala cha Jubilee.

Maelezo ya video,

Martin atamchagua rais mara ya kwanza Kenya

3. Simeon Maranga, 22, ni kijana ambaye anawania kiti cha mwakilishi wa wadi ya Nkaimurunya, Kajiado akiwa mgombea huru ingawa anaunga mkono muungano wa upinzani NASA.

Maelezo ya video,

Simeon atamchagua rais mara ya kwanza Kenya

Alhamisi 03 Agosti, 2017

Beatrice: "Kumaliza siasa za pesa Kenya ni jambo ngumu sana. Hapo jana, Rais Uhuru aliwafokea watu wa Makueni kwa sababu ya kuiimba nyimbo za kusifu muungano wa upinzani NASA. Alisikika akiwa mwenye hasira. Ni jambo lililotarajiwa kwani, vile vile ndivyo Wakenya wamechoka kwa miezi sasa wakiwa bila chakula cha kutosha. Inawezekana kuwa, pesa zilizomwagwa pale kablaya msafara wa Uhuru Kenyatta kufika sio kidogo, ndiposa akakasirika. Isitoshe zile nyimbo za kumsifu Odinga. Sio kusema kwamba mrengo wa NASA ndio suluhisho la uongozi Kenya lakini ni vyema Wakenya kutupilia mbali hongo hizi, ili kuweza kubaini vyema uongozi unaofaa. Hizi pesa kidogo, mavazi ya kisiasa, iwapo utatokea ama hutatokea kwenye msafara mtaziona tu mara moja kwa miaka mitano. Wakenya mtaendelea kulipia kupitia bunge. Nataka kumbukusha kila Mkenya kwamba, NASA na jubilee ni magari mawili tu, yalizotoka kiwanda kimoja, Na madereva wawili tofauti. Ni vyombo tu vya kuwafikisha waendako, lakini sio mwendako kama Wakenya."

Martin: "Nimehuzunika ambavyo mgombea mwenza wake Raila Odinga, Bw Kalonzo Musyoka anahusisha serikali na kifo cha Msando. Hivi ni vibaya mno maana inaweza kufanya vita vianze.

Hakuna mti amepanga kuiba kura na wakati huu naona Rais Uhuru Kenyatta atapata kura 61%+4. Hata hivyo jambo muhimu ni amani na upendo. Tukiwa na Uhuru na Raila au bila wawili hao, maisha bado yataendelea. Wakenya wote tuko kitu moja."

* Simeon bado hajatuma mchango wake

Jumanne 25 Julai, 2017

Simeon: Kukosa kuja kwa rais wa taifa katika mjadala wa taifa kumemkosesha nafasi ya kuitetea miaka yake mitano 'usingizini'.

Hii ina maana kwamba rais hakuwa na jinsi ya kutetea muhula wake wa kwanza.

Kukosa kutimiza malengo ya kupeana vipatakilishi katika elimu, ufisadi uliokithiri , kutotimiza ujenzi wa viwanja vitano vya kimataifa na gharama ya juu ya maisha ni mambo ambayo yameigubika serikali ya Jubilee.

Raila Odinga alichukua nafasi hiyo kueleza taifa jinsi atapunguza hasaa gharama ya maisha.

Hali ya maisha imekua ngumu kwa wananchi wengi kutoka chakula, nauli mijini na kodi ya nyumba.

Uchaguzi huu ni wa farasi wawili, Raila Odinga na Uhuru Kenyatta.

Wengine, ndio, wanaomba kura na wana sera lakini hawajavutia wananchi.

Sasa ni jukumu la wananchi kupima na kufanya uchaguzi kwa makini.

Vijana wengi wanatarajia serikali ambayo itabuni nafasi za kazi, kuimarisha elimu na kukuza teknolojia.

Beatrice: Uhuru Kenyatta kutoonekana kwake katika mjadala ni dhihirisho kwamba hana njaa ya Uongozi. Nikidhani aweza ishi vyema bila mamlaka. Hataki mamlaka.

Hayo ni kando na kutoulizwa maswali ya ukulima, Afya kati ya mengine, kuna la muhimu ambalo Wakenya hawajui twafaa kujua.

Pesa za kutekeleza manifesto hizi watatoa wapi?

Tayari kuna fedha nyingi sana za kulipa na mirengo yote haituambii watakapotoa hizi hela.

Mrengo Wa Third Way umedhihirisha vyema utakavyo punguza ushuru.

Martin: Ni siku nyingine ambayo maulana ametujalia.

Jumatatu usiku nilishangazwa vile ambavyo rais Uhuru Kenyatta alikosa kufika katika mdahalo wa urais.

Mimi nikiwa mfuasi wa Jubilee sikufurahishwa na lile jambo ingawaje huenda yuko na sababu zake na kisha sisi wote twajua yeye ndio uwezo mkubwa nchini.

Pia nampongeza mheshimiwa Raila Odinga kwa vile alihubiri amani na kuwatakia Uhuru na Ruto kila la heri.

Hivyo aliongea kama kiongozi na ninatarajia kuona akitimiza ahadi yake kuwa utakuwa mchezo wa kirafiki na akishindwa atakubali.

Hata hivyo, jinsi ambavyo aliangazia vile atakavyokabiliana na changamoto zinazotukumba hakuwaridhisha Wakenya.

Hivyo naona Jubilee wapewe miaka mitano mengine wakamilishe kazi waliyoanza .

Ijumaa 21 Julai, 2017

Beatrice: "Bado nafurahia uamuzi wa mahakama wa kufutilia mbali uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuzuia kupigwa chapa wka karatasi za kura ya urais. Hapa wameokoa muda wa Wakenya. Iwapo IEBC wangeshindwa kwenye hii kesi, mpanglio wa upigaji kura, kulingana na tarehe, haungeambatana na mwatakwa ya Katiba.

Nafikiri huenda ikawa, uadilifu wa IEBC ndio ulikuwa unajaribiwa hapa na NASA.

Huenda ikawa wangejitosa kwenye uwanjani na kusema kwamba IEBC haifaii kufanya uchaguzi Huu.

Matukio haya yangeenda hivi, Wakenya wangepata msukumo wa kutokuwa na imani na kuzua vita. Kungekuwa pia na semi kwamba karatasi za uchaguzi, zingefaa kichapishwa siku 60 mbele ya uchaguzi.

Hii ingeleta tumbo joto. Kwa ufupi, Wakenya sio wajinga, tunaona na kuweza kubaini nani wana nia ya kugawanya Wakenya, zaidi wakusudia kuleta ghasia hata mbele ya uchaguzi

chama cha ODM, katika mtandao wa Twitter, kimekiri kuwa, kiko tayari kuyakubali matokeo ya uchaguzi, bora yawe ya kuaminika.

Matamshi haya kwa njia nyingine, yanaweza eleweka kwamba, matokeo yatakuwa ya kweli iwapo mrengo wao ndio utashinda.

Je, ni haki tu kama yatawiana na matakwa ya mrengo huu?

La. Wakenya, ThirdWay ni njia mbadala inayokwambia wazi kuwa, Kenya sio ya mirengo hii miwili ila ni yako kama mpiga kura. Mrengo wa ThirdWay hauna shida yoyote ile ya uadilifu."

Martin: "Leo nafurahi vile ambavyo jana mahakama iliweza kuruhusu kampuni ya Al Ghurair kupicha chapa za kura ya urais. Pia leo mahakama imeruhusu kutumiwa kwa sajili ya karatasi kama njia mbadala iwapo mfumo wa elektroniki utafeli.

Hii inaonyesha kuwa huenda jaji wa mahakama kuu Odunga yuko na ajenda yake na anapendelea muungano wa Nasa kwa sababu zisizojulikana.

Ni vyema viongozi wa kisiasa wajue taifa la Kenya ni kuu kushinda mtu binafsi na wajue wakenya raundi hii hatuko tayari kupigana kwa sababu ya tofauti za kisiasa.

Mimi niko tayari kukubali matokeo yoyote, Jubilee tukishindwa ni sawa na tukishinda ningefurahi sana wenzetu wa NASA wakikubali. Hamna jambo tamu kama kuona viongozi wakikubaliana na kufanya kazi pamoja."

Simeon: "Ningependa kushukuru jamii ya kimataifa kwa kuweka macho katika uchaguzi wa Kenya. Ningeomba wajumbe hawa wasisitize uwazi katika uchaguzi wa tarehe nane Agosti. Mahakama imeshaamua kesi zilizokua na uzito na uwezo wa kuzuia ama kuchelewesha uchaguzi.

Sasa ni wakati wa tume ya IEBC kufanya matayarisho kabambe na kueleza Wakenya kwamba wako tayari kusimamia uchaguzi . Mwisho ni kwamba uchunguzi wafaa kufanywa wa tuhuma zilizotolewa na NASA za orodha ya askari ambao muungano huo unahofia watatumiwa kubadilisha matokeo ya uchaguzi. Jamii ya kimataifa inafaa kuchunguza tetesi hizo."

Alhamisi 20 Julai, 2017

Beatrice: "Nafikiri serikali ya Jubilee imebobea katika utumizi wa propaganda, kama njia moja ya kutuliza Wakenya na kuwaondoa katika hali ya kutoridhika na kuwapa imani bandia wakati huu uchaguzi unapokaribia.

Uamuzi wa rais na naibu wake, William Ruto kutotokea kwa midahalo ya uongozi, iliyotarajiwa kupeperushwa moja kwa moja kwenye runinga, iliwashangaza wengi na kuibua maswali na kauli mbalimbali. Baadhi ya Wakenya, walikiri kukosewa heshima na mirengo yote miwili. Walisema kwamba, wote wamekiuka sheria ya uhamasishaji wa umma mambo wanayohitaji kujua, kama ilivyoandikwa kwa katiba.

Kauli za kuwakashifu zikiendelea, Jubilee ilitangaza kwamba wanatarajia kuwa na mkutano katika ukumbi mmoja jijini Nairobi. Ni uamuzi mzuri, ila hapa ninainua mkono na kusema, mirengo mingine ikiketi kwenye mikutano mirefu ya kupanga hatua watakazozichukua, Jubilee wana haraka ya kutekeleza uamuzi wao."

Martin: "Ninashangaa jinsi muungano wa upinzani Nasa umeanza kumhusisha waziri wa mambo ya ndani na usalama Dkt Fred Matiang'i na wizi wa kura katika uchaguzi mkuu.

Sote twamjua Matiang'i ni mchapa kazi na anafanyanga kazi yake vinavyostahili. Kwa kufanya hivi, viongozi wa Nasa wanaonyesha wazi kwamba hawako tayari kwa uchaguzi mkuu wa Agosti. Nafikiri ni vyema Wakenya wapate kujua ya kwamba mambo haya muungano wa Nasa unaleta kila siku huenda yakafanya kuwe na joto kali la kisiasa na si vyema maana kunaweza kukatokea vita.

Ningefurahia zaidi iwapo waziri mkuu mstaafu Raila Odinga angefanya siasa zake kwa kuuza sera. Awaambie Wakenya alichofanya ulipikuwa katika serikali na atakachowafanyia."

Kwa Wakenya wenzangu, sisi tu ni kama mawe ambayo watu hutumia kuchuna maembe, mtu tu apatapo embe, jiwe linasahaulika, hivyo ni vyema tufahamu kuwa, baada ya uchaguzi, wanasiasa watatusahau.. Tudumishe amani."

Simeon: "Sijaridhishwa kamwe na jinsi wanasiasa wanavyojaribu kuzuia Wakenya wasishiriki uchaguzi tarehe 8 Agosti.Ni aibu sana kwa taifa kugubikwa na kesi kortini wiki mbili kabla ya uchaguzi, ambazo naamini zinapoteza muda. Wakati huu ni wa tume kujatayarisha kwa uchaguzi, kuandaa teknolojia inayofaa kutumika na kuhakikisha kwamba kila kitu kiko sawa.Waziri wa usalama na mambo ya ndani Dkt Fred Matiang'i ni mmoja wa washiriki katika siasa za Kenya na hafai kumzuia ama kumwelekeza refarii wa uchaguzi. Hali ya serikali kutishia na kulazimisha tume ya uchaguzi kufanya wanavyotaka wao ni ya kushangaza.

Dkt Matiang'i anafaa kujitenga na shughuli yote kuhakikisha kwamba kuna usawa kwa wahusika wote."

Jumatano 19 Julai, 2017

Beatrice: "Leo katika ziara yangu ya kutafuta riziki nimekutana na mmoja wa wanaowania kiti cha uwakilishaji mbunge katika eneo bunge la Kigumo, viungani mwa jiji la Nairobi.

Baada ya mazungumzo baina yangu naye, nimebaini kwamba, baada ya siasa, anayeibuka mshindi na kuwa ndiye atakayekuwa kiongozi katika cheo chochote kile, anahitaji kusikika na kuoneka katika vyombo vya habari.

Mwanasiasa huyo alijieleza kuwa mwoga ama asiyependa kuangaziwa sana katika vyombo vya habari. Nami nikajiuliza, je? Waweza kushinda kiti chochote kile bila kujulikana vyema? La. Ni wangapi kama yeye, ambao labda ni viongozi Wakenya wanahitaji, ambao hawana pesa ama jinsi ya kupata nafasi katika vyombo vya habari hupoteza nafasi ya kuongoza kwa sababu ya ufisadi?

Nilikuwa najadiliana haya naye nikiwa bado nakumbuka kisa cha mdahalo wa wagombea wenza ambao walisusia mdahalo huo. Ni mgombea mmoja pekee ambaye alijitokeza."

Martin: "Naona kwamba wana Nasa wamejitahidi ili siku ya uchaguzi mkuu iahirishwe. Hii inajitokeza wazi kwanba hawako tayari hata kidogo kwa uchaguzi. Mwangi ambaye ni wakili wa chama cha ODM yumo mahakamani akiwawakilisha dhidi ya IEBC (Tume ya uchaguzi). Kama hawako tayari naona ni vyema waache kusumbua nchi wawaruhusu ambao wako tayari kuendelea na hizi mbio. Naona serikali ya Jubilee iko sawa kabisa. Raila Odinga (mgombea wa upinzani) anafanya siasa za kupiganisha Wakenya akisema kwamba iwapo uchaguzi utafanyika kwa njia ya haki, lazima atashinda. Naamini hii ni kuonyesha wazi kwamba iwapo atashindwa, atasema kuwa uchaguzi haukufanyika kwa haki na kwamba kura ziliweza kuibiwa."