Hoteli mbili zafungwa Nairobi kufuatia mlipuko wa kipindupindu.

Nairobi
Image caption Nairobi

Hoteli mbili zimefungwa mjini Nairobi kutokana na mlipuko wa ugonjwa kipindupindu mjini humo.

Wizara ya afya ilitoa amri ya kufungwa hoteli hizo kufuatia watu kadha wakiwemo mawaziri wawili kulazwa hospitalini, baada ya kula chakula kilichokuwa kimepikwa na hoteli hizo mbili.

Watu wanne tayari wamefariki kutoka na ugonjwa wa kipindupindu tangu mwezi Mei na zaidi ya visa 300 vya ugonjwa huo vimeripotiwa.

Waziri wa afya Dr. Cleopa Mailu anasema hoteli hizo mbili zitasalia zimefungwa hadi zitimize viwango vipya vya wizara ya afya.

Wizara ya afya pia ilifuta leseni za sehemu zote za kupika chakula kote nchini, na kubuni jopo litakaloongoza hatua za serikali dhidi ya ugonjwa huo.

Vituo sita vya kutoa matibabu vimebuniwa hasa maeneo ya mabanda mjini Nairobi kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindu.