Msemaji wa mawakili wa Trump ajiuzulu

Rais Trump

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais Trump

Msemaji wa mawakili wa rais Donald Trump amejiuzulu, kulingana na vyombo vya habari.

Mark Corallo alikuwa msemaji wa Marc Kasowitz ambaye anamtetea Trump katika uchunguzi kuhusu Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani na kumsaidia rais huyo kupata ushindi.

Ripoti zinasema kuwa bwana Corallo alitofautiana na mipango ya mawakili wa Trump kuwadharau na hata kupunguza uwezo wa maafisa wanaoongoza uchunguzi huo.

Hakujakuwa na tamko lolote kutoka kwake ama hata mawakili hao wa Trump.

Bwana Corallo ni mwandani wa wakili wa idara ya haki Robert Mueller ambaye anaongoza uchunguzi huo dhidi ya Urusi na amemsifu hadharani kulingana na mtandao wa politico.

Afisa huyo amekatishwa tamaa na operesheni za mawakili hao mbali na kambi pinzani zilizopo, ripoti hiyo imeongezea.

Bwana Mueller amewaajiri watu maarufu kujiunga na kundi lake, ambalo linachunguza iwapo kulikuwa na ushirikiano wowote kutoka kwa kundi la Trump ambao Urusi na rais Trump amekana kuwepo.