Upinzani wapoteza kesi nyengine ya uchaguzi Kenya

Kiongozi wa muungano wa Nasa nchini Kenya Raila Odinga akihutubia vyombo vya habari

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kiongozi wa muungano wa Nasa nchini Kenya Raila Odinga akihutubia vyombo vya habari

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA umepoteza kesi nyengine dhidi ya tume ya uchaguzi nchini humo IEBC.

Muungano huo unaoongozwa na kiongozi wa upinzani na mgombea wa urais Raila Odinga ulipoteza ombi ulilowasilisha mahakamani ukitaka uchaguzi kusitishwa katika kaunti zilizoathirika ama wadi iwapo mfumo wa kielektroniki wa kupiga kura utafeli.

Katika ombi hilo, Nasa ilihoji kwamba tume ya IEBC ilifeli kuweka mfumo mahsusi kama inavyohitajika kisheria.

Upinzani ulitegemea kifungu cha 55 cha sheria ya uchaguzi ambacho kinaikubali IEBC kuahirisha uchaguzi hadi pale mfumo mahsusi wa kupigia kura utakapowekwa.

Lakini Jaji Kanyi Kimondo, Hedwig Ong'udi na Alfred Mabeya waliipinga kesi yao wakisema IEBC imeweka mikakati ya kukabiliana na tatizo la kufeli kwa mfumo huo wa upigaji kura.

Walikubaliana na IEBC kwamba tume hiyo imeweka mikakati ya kukabiliana na utambulizi wa wapiga kura na urushaji moja kwa moja wa matokeo iwapo mfumo huo utafeli.

Kulingana na majaji hao Nasa ilishindwa kuelezea kesi yao na kuongezea kwamba ombi hilo pia linaweza kuliweka taifa hilo katika hali ya switofahamu