Uchaguzi Kenya 2017: Mfahamu mgombea urais Japheth Kavinga Kaluyu

Japheth Kaluyu

Kwenye tovuti yake, na unapokutana naye, anajieleza kama mtu mwenye ndoto kuu, na kwa kweli kutaka kuwa rais wa taifa kama Kenya ni ndoto kuu.

Dkt Japheth Kavinga Kaluyu anasimulia alivyozaliwa katika kijiji kidogo Afrika na kuchunga ng'ombe malishoni. Wakati huo alikuwa na ndoto ya kuwamiliki ng'ombe na mbuzi na kuwa na uhuru wa kuwapa majina kutokana na tabia zao.

Anaeleza alivyofurahia kuogelea kwenye mto na vidimbwi vya maji mifugo wake wakikata kiu.

Lakini sasa ndoto yake ilibadilika kadiri alivyokua na sasa ni msomi Marekani na mhamasishaji.

Anasema jambo analojivunia zaidi kwa sasa ni kuwasaidia watu kutimiza ndoto zao.

Dkt Kaluyu, ambaye anawania urais akiwa mgombea huru, alizaliwa katika "kijiji kidogo maskini" eneo la Kakuuni, Kitui mashariki mwa Kenya mwaka 1965.

Mgombea mwenza wake ni Eliud Muthiora Kariara, ambaye aliangaziwa sana baada ya kujitokeza peke yake kuhudhuria mdahalo wa wagombea wenza wa urais uliokuwa umeandaliwa na vyombo vya habari 17 Julai.

Maelezo ya picha,

Mgombea mwenza wa Dkt Kaluyu, Eliud Kariara

Dkt Kaluyu alisomea elimu ya msingi katika shule ya Katulani na baadaye akajiunga na shule ya Mtakatifu Charles Lwanga katika eneo la Kitui.

Alihamia nchini Marekani na akahitimu na shahada ya masuala ya fedha na uchumi mwaka 1995, na baadaye akasomea shahada ya pili katika fani iyo hiyo.

Alisomea shahada ya uzamifu katika sera na utafiti kuhusu afya mijini, akiangazia zaidi kuhusu Virusi vinavyosababisha Ukimwi, na kuhitimu mwaka 2010.

Kuanzia mwaka 2000, kwa miaka sita, anasema alifanya kazi Wall Street jijini New York.

Baada ya kufuzu na shahada ya uzamifu na kuanza kufundisha chuo kikuu, alifanywa kuwa mkuu wa kitivo katika Chuo Kikuu cha Strayer nchini Marekani mwaka 2012 na mwaka 2013 akawa profesa katika vyuo vikuu kadha.

Ameandika vitabu viwili vya kuwahamasisha watu na kuwashauri jinsi ya kufikia ufanisi, Succeeding in the Face of Challenge (Kufanikiwa ukikabiliwa na changamoto), na Timing- Engaging when it matters most (Wakati, kuchukua hatua wakati ufaao zaidi).

Kuanzia mwaka 2016, alianza kushiriki katika vipindi vya redio na runinga.

Kuanzia mwaka 2010, amekuwa pia akifanya kazi ya ushauri na kutoa mafunzo kwa mashirika mbalimbali.

Dkt Kaluyu anasema hajawahi kuwania wadhifa wowote wa kisiasa awali, ingawa alijitosa kuwania nyadhifa mbalimbali katika taasisi na mashirika aliyofanya kazi.

Anasema alianza kufikiria kuwania urais kwa mara ya kwanza miaka mitano iliyopita.

Kunao wanaosema kwamba yeye hajakuwa akiishi Kenya na hivyo hayafahamu vyema matatizo ya Kenya.

Lakini anakanusha hayo: "Nimezuru Kenya mara 10 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita".

Anasema kando na kufahamu yanayojiri Kenya, safari ambazo amekuwa akizifanya kufika Kenya zinaashiria kujitolea kwake kwa taifa lake la kuzaliwa.

Nembo yake ni kifaa cha kuzima moto na kauli mbiu yake ni 'Tuko Masaa'. Dkt Kaluyu amesema akichaguliwa kuwa rais, atazima moto wa matatizo yote yanayokumba Kenya.

Kampeni yake ameipa jina Badilisha Kenya Movement na ana vipaumbele sita: kupunguza gharama ya maisha, kuunda nafasi za ajira, kutoa mafunzo, kupunguza kodi, kumaliza ulaji rushwa na kuwekeza katika raia wanaoishi nje ya nchi.

"Kisa changu ni sawa na cha wavulana na wasichana wengi Kenya na Afrika kwa jumla. Ndoto zao zinazimwa na watu walio na pesa na wenye mamlaka. Wamegeuzwa kuwa watazamaji," anasema.

"Safari yangu inaanza kuleta mabadiliko sio tu kwa taifa letu bali pia kuanzisha wimbi la mabadiliko kwa kizazi hiki Afrika. Kuwasaidia kujenga mustakabali wao.".