Majaliwa awataka waliojenga mpaka wa Tanzania na Zambia kubomoa nyumba zao

Bw Majaliwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Watu waliojenga ndani ya eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia wamepewa muda wa miezi mitatu kubomoa nyumba zao na kuondoka maeneo hayo.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanza kuweka alama za X katika nyumba 252 zilizojengwa ndani ya mpaka huo ili wahusika wazibomoe.

Bw Majaliwa, aliyetembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na Zambia, amesema waliojenga kuanzia umbali wa mita 50 kutoka Tanzania na mita 50 kutoka Zambia wabomoe nyumba hizo kwa hiari.

Kituo hicho kinajengwa na Serikali ya Tanzania na kitagharimu sh. bilioni 12 za Tanzania.

"Kuna watu wamejenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia na kuendesha biashara zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linazikosesha Serikali mapato," amesema.

"Hatuna msamaha kwa watu waliojenga katika eneo hili kwa sababu wamesababisha tupoteze kodi nyingi, hivyo baada ya kumalizika muda huo mamlaka husika zibomoe nyumba zote zitakazosalia."

Bw Majaliwa awali alikutana na Mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini Zambia, Bw. Field Simwinga ambaye alisema wamekubaliana na utekelezaji wa agizo hilo kwa kuwa jambo hilo linaathiri shughuli za mipakani kwa pande zote mbili.

Bw Simwinga alisema tayari wameshaanza kuwaeleza wananchi wao waliojenga ndani ya mpaka huo kuanza kuondoka.

Waziri mkuu wa Tanzania amesema wanataka eneo hilo liwe wazi ili iwe rahisi kuutazama mpaka huo kwa umakini.