Nani ana nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi mkuu Kenya 2017?
- Peter Mwai
- BBC Swahili

Chanzo cha picha, AFP
Bw Kenyatta na Bw Odinga waliwania tena mwaka 2013
Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (NASA) ulipomtangaza mgombea wake wa urais, na mgombea mwenza katika mkutano ukumbi wa Bomas Nairobi mwezi Aprili, kinyang'anyiro cha kipekee kilianza kujisuka.
Kwa kumtangaza aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwa mgombea mwenza na makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka kuwa mgombea mwenza wake, upinzani ulikuwa umehakikisha uchaguzi wa Agosti mwaka huu utakuwa kama marudio ya uchaguzi wa mwaka 2013.
Bw Odinga, akitumia muungano wa Coalition for Reform and Democracy (Cord), wakiwa na Kalonzo, walishindana uchaguzini dhidi ya muungano wa Jubilee wake Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.
Wagombea wengine ni Cyrus Jirongo wa United Democratic Party (UDP), Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance, Abduba Dida wa Alliance for Real Change (ARC), na wagombea huru Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japheth Kavinga.
Wanachojiuliza watu ni iwapo kunafaa kutarajiwa matokeo tofauti na ya Machi mwaka 2013, Bw Kenyatta alipopata asilimia 50.7 ya kura, naye Bw Odinga akapata 43.31.
Wanaoamini kwamba hakuwezi kutarajiwa matokeo tofauti, walikuwa miongoni mwa waliopinga Bw Odinga kuteuliwa kuwa mgombea wa muungano wa upinzani.
Walitaka kuwe na mgombea tofauti ambaye 'angesisimua' upya hamu ya wapiga kura wenye imani na upinzani.
Msimamo sawa, japo bila shaka kwa sababu tofauti, ulionekana kuwepo miongoni mwa mrengo wa serikali.
Aliyeongoza ni Bw Ruto ambaye baada ya kutangazwa kwa mgombea wa upinzani, alisema: "Eti ile wametuletea ni ile ile ya 2013. Sasa, hii jameni ni utapeli wa aina gani. Sisi tulikuwa tunangojea walitwambia wako na maajabu, wako na miujiza. Tulikuwa tunafikiria wameenda kutoa mgombea nje ya nchi, kumbe ni wale wale tuliwashinda 2013.
"Kama hawa, kwa sababu Raila ni yule yule, Kalonzo ni yule yule, Musalia (Mudavadi) ni yule yule .Hawa watu si tunawanyorosha asubuhi na mapema, hata kama ingewezekana tungewaambia sasa IEBC wasongeze uchaguzi ikuwe karibu," alisema akiwa mjini Thika.
"Ni nini iliwazuia wangesema marudiano ya 2013 ni 2017, kivumbi tuliwaonyesha siku ile tutawaonyesha kivumbi pamoja na moshi."
Walio na msimamo sawa, wanaamini safari itakuwa rahisi kwa Bw Kenyatta na wenzake kwani ukijumlisha kura alizopata Bw Odinga na zile alizopata Bw Mudavadi, ambayo sasa yumo kwenye muungano wa upinzani, hazitoshi kuwawezesha kuishinda serikali ya sasa.
Bw Kenyatta alipata kura 6,173,433 naye Bw Odinga akapata 5,340,546 mwaka 2013. Bw Mudavadi alijizolea kura 483,981. Ukazijumlisha, Bw Kenyatta akiwa na 50.7, asilimia ya Bw Odinga na Bw Mudavadi kwa pamoja itakuwa ni 47.24.
Lakini hali kwamba upinzani uliungana, tofauti na ilivyotarajiwa kwamba umoja wao ungesambaratika, unazua uwezekano kwamba kwa pamoja huenda wakafanya vyema kuliko awali.
Wanasiasa kuhama vyama vya upinzani
Bw Kenyatta ana nafuu nyingine, kwamba kuna baadhi ya magavana na wabunge walioshinda uchaguzi mwaka 2013 ambao wamehamia katika muungano wake, baadhi kutoka maeneo ambayo kura zinashindaniwa maeneo ya Pwani na Magharibi.
Mfano eneo la pwani Salim Mvurya (gavana wa Kwale), Hussein Dado (gavana wa Tana River), Gideon Mung'aro (mbunge wa Kilifi Kaskazini). Manaibu gavana Kenneth Kamto (Kilifi) na Hazel Katana (Mombasa), Fatuma Amani (Kwale) pia walihamia Jubilee.
Mwakilishi wa wanawake Taita Taveta Joyce Lay alihamia Jubilee na sasa anawania useneta, seneta wa jimbo hilo Dan Mwazo naye pia akahamia Jubilee na sasa anawania ugavana.
Kuna wasemao hata hivyo kwamba kuhama kwa viongozi si kwamba wamehama na wafuasi wa chama na kwamba huenda wapiga kura wakawa bado walisalia katika chama chao cha asili.
Samahani, kisakuzi chako hakiwezi kuonesha ramani hii
Isitoshe, wapo waliokuwa upande wa serikali Pwani lakini wakashindwa na wakati huu wamehamia upinzani. Mfano ni waziri wa zamani Chirau Ali Mwakwere aliyeunga mkono Bw Kenyatta mwaka 2013 lakini akashindwa. Bw Kenyatta alimteua kuwa balozi wa Kenya nchini Tanzania. Lakini sasa mwanasiasa huyo anawania ugavana jimbo la Kwale kupitia chama cha Wiper, chake Bw Musyoka.
Maeneo ya kushindaniwa
Kwa kuangalia uungwaji mkono wa mirengo yote miwili kisiasa, maeneo ambayo hakuna mrengo mmoja uliopata zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa mwaka 2013, ni ishara kwamba kunaweza kukatokea mabadiliko fulani.
Majimbo ambayo hakukutokea mbabe wa moja kwa moja ni pamoja na jiji kuu Nairobi, Lamu, Garissa, Wajir, Marsabit, Isiolo, Samburu, Trans Nzoia, Narok, Kajiado, Vihiga, Bungoma na wapiga kura nje ya nchi.
Nini kitaamua nani atashinda?
Ndipo mgombea aweze kutangazwa mshindi, mwaniaji ni lazima awe amepata kura angalau moja juu ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa. Kwa kufuata matokeo ya mwaka 2013, ambapo Rais Kenyatta alishinda kwa asilimia 50.7 kunaweza kukatokea mabadiliko kwa kutegemea idadi ya wapiga kura watakaojitokeza katika maeneo mbalimbali, ngome za kila mgombea na maeneo ya kushindaniwa.
Kwa kuangalia upigaji kura wa mwaka 2013, kuna maeneo ya Pwani kwa mfamo Mombasa na Kilifi ambapo idadi ya waliojitokeza ilikuwa asilimia 66 na 65 mtawalia. Katika maeneo hayo mawili, Bw Odinga alipata asilimia 70 na asilimia 84 ya kura zilizopigwa. Hiyo inaashiria uwezekano kwamba iwapo watu wengi zaidi wangejitokeza maeneo hayo - iwapo upigaji kura ungefuata mtindo wa waliojitokeza- huenda kura zake zingeongezeka.
Mtafiti mkuu katika kampuni ya Ipsos Tom Wolf, alipokuwa anatoa matokeo ya utafiti wa maoni wa kampuni hiyo 23 Julai, alidokeza kwamba kiwango cha kujitokeza kwa wapiga kura kitachangia sana kuamua nani ataibuka mshindi kati ya Bw Kenyatta na Bw Odinga.
Bw Wolf anaamini mshindi atapatikana katika duru ya kwanza.
Matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni mbalimbali yanaonekana kutofautiana.
Matokeo ya karibuni zaidi (Julai 23) ya Ipsos Kenya yasema Bw Kenyatta anaongoza akiwa na asilimia 47 naye Bw Odinga ana asilimia 43. Ipsos wanasema asilimia 5 hawajaamua watampigia nani kura. Hao wengine hawatapiga kura au watampigia wagombea hao wengine. Kwa kulinganisha na matokeo ya utafiti yaliyotolewa mwishoni mwa Juni, rais ameshuka kwa asilimia moja naye Bw Odinga akaimarika kwa asilimia moja.
Matokeo ya kampuni ya Infotrak yaliyotolewa siku iyo hiyo hata hivyo yanaonesha Bw Odinga anaongoza akiwa na asilimia 47 naye Bw Kenyatta akimfuata akiwa na asilimia 46. Kwa mujibu wa Infotrak, asilimia 6 hawajaamua watamuunga nani mkono.
Mkuu wa Infotrak pia anasema uwezekano wa kukosekana mshindi awamu ya kwanza ni finyu mno.
Charles Hornsby mwandishi wa kitabu kwa jina Kenya: A History since Independence, (Kenya: Historia ya tangu uhuru) kwenye utathmini wake mtandaoni anasema baada ya kuzingatia idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura, asili ya wapiga kura na mtindo wa upigani kura, Bw Kenyatta ana nafasi nzuri ya kushinda katika awamu ya kwanza.
Anakadiria kwamba kitaifa kiwango cha kadiri cha wapiga kura asilimia 83 watajitokeza, maeneo kama vile Kati na Nyanza yakiwa juu hadi asilimia 90 na mengine mfano Mombasa, Kilifi na Kwale yakishuhudia viwango vya chini vya wapiga kura kujitokeza vya hadi asilimia 65.
Hata hivyo, mwenyewe pia anakiri kwamba ni vigumu kubashiri hasa wapiga kura watajitokeza kwa kiwango gani.
Samahani, kisakuzi chako hakiwezi kuonesha ramani hii
Idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kila kaunti Kenya 2017
Takwimu za kufikia tarehe 31 Julai 2017.